……………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu, DSM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amefungua Mashindano ya Ulimwende ya Vyuo Vikuu (Miss High Learning 2021) usiku wa Septemba 25, 2021 na kuwahakikishia washiriki na wadau wote wa urembo kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuboresha eneo la sanaa ya urembo ili kuibua vipawa na vipaji vya wasanii hatimaye waweze kunufaika.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo kwenye hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam ambapo amesisitiza kuwa urembo ni sanaa muhimu inayotoa ajira duniani hivyo washiriki wake wanatakiwa kujiamini na kuzingatia maadili ya taaluma hiyo ili waweze kufika mbali na kunufaika nayo.
“Mashindano ya urembo kwa Vyuo Vikuu ni miongoni mwa mashindano makubwa hapa nchini hivyo sisi kama Wizara inayosimamia Sekta ya Sanaa tumejipanga vizuri kushirikiana na waandaaji ili kuyapa heshima inayostahili”. Amefafanua Dkt. Abbasi
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuinua Sekta ya Sanaa nchini na ndio maana imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasaidia wasanii ikiwa ni pamoja na kuwaanzishia Mfuko maalum wa Maendeleo ya Sanaa ambao utatumika kuwawezesha wasanii kwenye kazi zao.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha mapenzi makubwa katika sanaa na michezo ametoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni,” Amesisitiza Dkt. Abbasi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi michango mikubwa iliyotolewa na Serikali katika kipindi hiki kwenye tasnia ya Sanaa na michezo ni pamoja na kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 9.5 kwa ajili ya kujenga viwanja vya wazi vya michezo kwa ajili ya wasanii na wanamichezo.
Pia amesema Serikali inakusudia kujenga ukumbi wa kisasa (Arts & Sports Arena) utakaokuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya watu elfu kumi na tano kwa mara moja kwa ajili ya kusaidia kuweka michezo mbalimbali kwenye ukumbi huo ambapo amefafanua kuwa michoro ya ukumbi huo ipo mbioni kukamilika na ikikamilika itapelekwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi.
Ameongeza kuwa katika kuboresha miundombinu ya michezo ikiwemo sanaa Serikali imesamehe kodi ya nyasi bandia za viwanja vya michezo na kutaka asilimia tano ya mapato ya kwenye michezo ya kubahatisha kwenda katika mfuko wa kuendeleza michezo hapa nchini.