……………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, DSM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi usiku wa Septemba. 25, 2021,ametoa zawadi na kufunga Shindano la Bingwa lililowaweka pamoja vijana wenye vipaji mbalimbali ndani ya jumba moja kwa siku 75.
Shindano hilo lililoandaliwa na Kampuni ya Startimes na kuoneshwa kupitia luninga ya TV3.
Amewasihi walioshiriki wote wa shindano hilo kutumia vyema mafunzo waliyoyapata kuboresha maisha yao.
Meneja Masoko na Mahusiano wa Star Times Tanzania Juma Sharobaro amefafanua kwamba katika kipindi chote ambacho washiriki wamekuwa kwenye jumba hilo walipata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali kuhusu kazi zao za sanaa, namna ya kutumia vyema mitandao ya kijamii na stadi nyingine za maisha.
Aidha, Dkt. Abbasi ameipongeza Kampuni hiyo kwa kuanzisha shindano hilo ambalo limewakutanisha vijana toka sehemu mbalimbali nchini na kuwapa fursa za kuongeza ujuzi utakaowasaidia kwenye maisha yao.
“Nawapongeza Star Times kwa ubunifu huu wa kipekee kwani mmetoa fursa kwa vijana na nimefurahi kusikia kila mshiriki aliyetoka kwenye shindano hili aliweza kupata kitu cha kumsaidia kwenye maisha yake,” aliongeza Dkt. Abbasi.
Kwa upande wake Meneja Masoko na Mahusiano wa Star Times Tanzania Juma Sharobaro ameishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono huku akiongeza kuwa shindano hilo litawainua vijana kiuchumi.
Katika shindano hilo, Joel Revocatus(Photogenic) ameibuka mshindi na kujinyakulia zawadi ya fedha za kitanzania shilingi milioni 10 na gari jipya.
Ameishukuru Serikali ya chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya Sanaa.