NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amewataka Maafisa Ugani wa Halmashauri zote Nchini kutoa elimu ya kilimo bora na ufugaji mzuri ili wananchi wawe na uelewa wa wanachotaka Kwenda kukifanya kabla ya kwenda kuchukua mikopo kwenye Taasisi za kifedha.
Ndejembi ametoa kauli hiyo leo wilayani Meru mkoani Arusha wakati akikabidhi hati 15 kwa wananchi wa Vijiji vya Maweni na Kirangai vilivyopo Kata ya Kikwe ambapo wananchi wake walifanyiwa urasimishaji wa maeneo yao kwa msaada wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA) na jumla ya mashamba 1607 yalipimwa kati yao 889 yakikatiwa hati zake na hati ambazo zimeshachukuliwa ni 494.
Akizungumza na wananchi wa Vijiji hivyo baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye masjala mbili za vijiji hivyo zilizojengwa na MKURABITA ambazo zimegharimu kiasi cha Sh Milioni 102, Naibu Waziri Ndejembi amewataka wananchi kujitokeza kupeleka taarifa zao ili waweze kufanyiwa urasimishaji wa maeneo yao jambo ambalo pia litawawezesha kuomba mikopo kwenye Taasisi mbalimbali za kifedha ambayo itawasaidia kuendeleza maeneo yao au kuwekeza katika biashara.
“Mkakati huu wa MKURABITA wa kuwezesha urasimishaji wa maeneo umekua ni msaada mkubwa kwa wananchi wetu, ndani ya Wilaya hii ya Meru Watu Tisa wamechukua kiasi cha Sh Bilioni 1.3 kama mkopo baada ya kupimiwa ardhi zao na kupatiwa hati, mkopo huu ni kwa ajili ya kuendeleza mashamba yao, biashara zao.
Nitoe wito kwenu wananchi mkisharasimisha ardhi yenu mfanye kazi kwa karibu na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na hii niwatake kabisa Maafisa Ugani kutoa elimu kwa wananchi hawa ya kilimo bora, ufugaji mzuri ili wanapoenda kuchukua mkopo wawe tayari na uelewa wa kitu wanachoenda kufanya,” Amesema Naibu Waziri Ndejembi.
Ametoa wito kwa wananchi wa Vijiji hivyo kujitokeza kwa wingi kufanya urasimishaji wa maeneo yao pindi masijala hizo zitakapokamilika huku akiahidi kwamba Serikali kupitia MKURABITA itaendelea kuongeza maeneo yake ya kufanya kazi na kupima ardhi.
“Katika kuhakikisha hatuna migogoro ya ardhi katika maeneo yetu kuwa na hati hizi kunamaanisha unakua na uhakika na eneo lako wewe pamoja na vizazi vyako kwa sababu hati hizi zitahifadhiwa kwenye masjala hizi tunazojenga hivyo niwaombe wale ambao wanachukulia jambo hili kirahisi wajitokeze kwa wingi kwenda kurasimisha ardhi zao,”Amesema Ndejembi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MKURABITA, Dk Seraphia Mgembe amesema wataendelea kujenga masjala hizo sehemu mbalimbali nchini ili kuweza kusaidia uwezeshaji wa zoezi la urasimishaji wa maeneo kwa wananchi.
” Tunawashukuru wananchi wa Kata hii ya Kikwe na haswa Vijiji hivi vya Maweni na Kirangai kwa ushirikiano mkubwa waliotupa katika kufanikisha ujenzi wa masjala hizi, wamekua wakijitoa katika kusaidia ujenzi wake na zaidi kuwa walinzi wa vifaa vya ujenzi, tunaamini kukamilika kwake kutasaidia kumaliza changamoto za ardhi kwenye vijiji hivi,” Amesema Dk Mgembe.