Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na viongozi wakuu wa utawala wa Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara yake, wakati alipokuwa akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira mpya za askari 2,300 kwa Vyombo hivyo, jijini Dodoma, leo Septemba 24, 2021. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (meza kuu) akimsikiliza Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Lulu Zodo alipokuwa akizungumza katika kikao chake na viongozi wakuu wa utawala wa Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara yake, wakati alipokuwa akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira mpya za askari 2,300 kwa Vyombo hivyo, jijini Dodoma, leo Septemba 24, 2021. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
*****************************
Na Felix Mwagara, MoHA, Dodoma.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira mpya za askari 2,300 kwa Vyombo vyote vya Usalama vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Akizungumza katika kikao chake na viongozi wakuu wa utawala wa vyombo hivyo, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara, Mtumba, jijini Dodoma, leo, Waziri Simbachawene alisema ofisi yake imepokea barua kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuhusu ajira mpya.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa ajira mpya kwa vyombo vya usalama vilivyo chini Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ametupatia Jeshi la Uhamiaji nafasi 350 kwa kada ya Konstebo, lakini pia ametupatia nafasi 700 kwa Jeshi la Magereza kwa nafasi za ‘Warder’ na ‘Wardress’, pia ametupatia nafasi 250 kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kada ya Konstebo, na pia ametupatia nafasi 1,000 kwa Jeshi la Polisi kwa kada ya Konstebo,” alisema Simbachawene.
Waziri Simbachawene alisema kwa niaba ya Wizara yake pamoja na vyombo anavyoviongoza amemshukuru Rais Samia kwa kutoa nafasi hizo ambazo zitapunguza kwa kiasi kikubwa ukosefu wa askari katika vyombo hivyo.
“Napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Wizara na Vyombo hivi ambavyo Wizara yetu inavisimamia kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia nafasi hizi, pamoja na changamoto tulizokuwa navyo, suala la upungufu wa askari lilikua jambo ambalo linatupa changamoto, na uzuri ni kwamba kibali kilichokuja kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kimeelekeza kabisa tuajiri askari wa ngazi ya chini,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, askari hao ndio watakuwa wapiganaji, wapambanaji, na anatarajia kuwa vyombo hivyo katika mchakato wake vitazingatia maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha kwamba watakaopata nafasi hizo ni wale waliopitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kupata malezi na kuhitimu lakini pia walishiriki katika kujenga nchi kupitia JKT.
Pia alisema kama kutakua kuna namna yoyote tofauti na sifa hizi zitatolewa na vyombo vyenyewe katika kutangaza nafasi hizi katika maeneo yao.