Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo akiongea na watumishi wa Chuo cha Katumba FDC na Wizara ya Elimu Makao Makuu (hawapo pichani) wakati alipotembelea chuo hicho hivi karibuni.
Mkuu wa chuo cha Katumba FDC, Mussa Mturuck (aliyesimama) akisoma taarifa ya chuo hicho mbele ya Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo (aliyekaa).
Muonekano wa baadhi ya majengo yaliyokarabatiwa katika chuo cha Katumba FDC kilichopo Tukuyu mkoani Mbeya.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo (wa nne kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Chuo cha Katumba FDC na Wizara ya Elimu Makao Makuu
……………………………………..
Na.Mwandishi Wetu,Tukuyu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo ameutaka uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Katumba (FDC) kuongeza kozi wanazotoa chuoni hapo kwa kuzingatia mahitaji halisi ya jamii ya eneo hilo.
Ameyasema hayo wilayani Tukuyu mkoani Mbeya hivi karibuni alipofanya ziara chuoni hapo ambapo amesema malengo makuu ya vyuo hivyo ni kuboresha jamii ya eneo husika.
Amewataka kuangalia mahitaji yaliyopo katika eneo hilo ili waweze kuanzisha kozi ambazo zitatatua changamoto za jamii ya eneo hilo.
“Inabidi tuangalie huku Tukuyu kuna mahitaji gani mengine ambayo tunaweza tukaanzisha kozi ambazo zitasaidia wananchi wa eneo hili,” amefafanua Prof. Nombo
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka kuanzisha kozi ambazo zitaongeza thamani kwa mazao ambayo tayari yanalimwa katika eneo hilo.
“Mfano hapa mnalima viazi na ndizi, kuliko kupeleka kuuza maeneo mingine mngefikiria kuwa na kozi ambazo zitaongeza thamani ya mazao hayo yakiwa hapa hapa kwenu,” amesisitiza Prof. Nombo.
Awali akitoa taarifa ya chuo hicho, Mkuu wa chuo, Mussa Mturuck amesema kabla ya maboresho ya miundombinu yaliyogharimu zaidi ya Shilingi milioni 600, chuo kilikuwa na wanafunzi 250 na sasa kina jumla ya wanafunzi 401.
Ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uboreshwaji wa miundombinu na kuahidi kuitunza kwa kushirikiana na uongozi na wanachuo.
Aidha, Mturuck amemuahidi Naibu Katibu Mkuu Nombo kufanyia kazi maagizo yake ambapo amesema tayari wako katika mpango wa kuanzisha kozi za kilimo cha mboga na matunda, uchomeleaji vyuma na udereva wa magari.
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Katumba kinatoa mafunzo kwa wanafunzi waliokosa fursa ya kusoma kwenye mfumo rasmi kwa sababu mbalimbali ikiwemo uyatima na ujauzito. Chuo hiki kinatoa kozi za Umeme wa majumbani, Umeme wa magari, Uhazili, Ushonaji, Ualimu wa Chekechea na Elimu ya sekondari kwa mfumo wa QT.