*********************************
NA MWANDISHI WETU, KATAVI
Katika kuadhimisha wiki ya kusafisha fukwe, wakazi wa kijiji cha Ikola kilichopo wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wamejitokeza kusafisha fukwe za ziwa Tanganyika na mwalo wa Ikola ili kuweka mazingira safi na kusaidia kuondoa taka ngumu za plastiki
Imeelezwa kuwa taka hizo zikiingia katika maji zinasababisha miale ya jua kushindwa kupenya katika maji na hivyo kuathiri viumbe maji wakiwemo samaki
Wakazi hao wamesema wameamua kujitokeza kufanya usafi baada ya kupata elimu ya madhara ya uchafu kwa samaki
‘Hii ni faida kwetu kwani kukiwa safi samaki hawatapata madhara na sie pia tutakuwa na uhakika wa kupata samaki wa kutosha’ alisema Saida Hassan
Akieleza madhara ya uchafu katika ziwa tanganyika mratibu wa mradi wa kuimarisha uvuvi kutoka Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa Hashim Muumin amesema uchafu unaathri viumbe maji
Amesema mradi huo ni wa miaka mitano unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya na Serikali ya Ujerumani na umelenga samaki aina ya mgebuka na dagaa ambapo unatekelezwa katika mikoa ya Kigoma Katavi na Rukwa
Ameongeza kuwa lengo la kufika kushirikiana na wakazi wa Katavi katika shughuli za usafi ni kuutambulisha mradi huo
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Tanganyika Afisa tarafa wa Karema Mboni Mpaye ametoa wito kwa jamii usafi kuwa endelevu