KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Wazee,Prof. Abel Makubi akizungumza katika kikao na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichofanyika leo September 23,2021 jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Wazee,Profesa Abel Makubi akisisitiza jambo kwa Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichofanyika leo September 23,2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia magonjwa yasiyoyakuambukiza kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali,Dkt.James Kihologwe,akizungumza katika kikao na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichofanyika leo September 23,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Wazee,Prof. Abel Makubi wakati akizungumza kwenye kikao na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichofanyika leo September 23,2021 jijini Dodoma.
…………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Wazee,Prof. Abel Makubi amesema Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa watapimwa utendaji kazi kwa mambo matano ambayo ni ukusanyaji wa mapato,uwajibikaji,uboreshaji wa huduma,jinsi wanavyotekeleza maagizo kutoka juu,ubunifu na kushughulikia malalamiko ya wagonjwa.
Akizungumza leo,Sepetemba 23,2021 katika kikao na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa,Prof.Makubi amesema wataupima utendaji kazi wa Waganga Wafawidhi katika Hospitali za Mikoa kwa kuangalia uwajibikaji,uongozi,uzalendo na ubunifu kwa kufanya vikao vingi na kushirikisha wafanyakazi katika mambo mbalimbali.
“Tutakuwa tunawapima jinsi gani unavyoboresha huduma zako mtu akifika anaona ubora.Pia mapato,unapoboresha mapato anafika ‘target’ yake na jinsi unavyoshughulikia malalamiko ya wananchi,niseme malalamiko mengi yamepungua sana, mwaka jana kila siku ilikuwa ni malalamiko sasa hivi yamebaki Wilayani yamepungua sana,”amesema
Pia amesema watawapima jinsi wanavyotekeleza maagizo kutoka juu mfano kutoka kwa Rais,Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wa juu pindi wanapotoa maagizo.
“Mwingine anapuuzia tu maagizo ya Rais au Waziri Mkuu,miongozo unayoletewa baada ya mwezi unaambiwa ulete ripoti huleti,Masuala ya ubunifu nayo tunayaangali,pia kutokugombana na wafanyakazi wenzako,tunategemea ninyi ndio mnajukumu kubwa la kubeba Mikoa kuhakikisha huduma zinakuwa bora pamoja na kuondoa malalamiko na nyinyi ndio wasimamizi wa hizo hospitali,”amesema Prof .Makubi
Katika hatua nyingine,Prof.Makubi amesema Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuendelea kuboresha huduma za tiba na kinga ikiwemo kupanua huduma za kibingwa katika Hospitali za Wilaya.
“Serikali awamu ya sita tumedhamiria kuboresha huduma za afya mahali ambako awamu ya tano imeishia,ujenzi wa vituo vya afya vingi vilijengwa na sasa hivi tuna vituo vingi vimeendelea kujengwa na havijakamilika na kuna ujenzi wa Hospitali za Wilaya hivyo tunaendelea hapo hapo.
“Maeneo ya msingi ni kuboresha na kupanua huduma za ubingwa katika hospitali za Rufaa za Mikoa,tungependa kuona kila mmoja akipiga hatua na ikiwezekana huduma za ubingwa bobezi tungependa kuona katika mikakati yenu mwaka huu mnalipa kipaumbele kwa maana ya kuwa na Madaktari bingwa na vitendea kazi na huduma ziweze kuwafikia,”amesema.
Amesema Wizara imejipanga kujikita zaidi katika ubingwa bobezi ili Hospitali za Kanda zibaki katika huduma za kawaida na kuvutia watalii ambapo hata mtalii akihitaji huduma aweze kupata.
“Nchi yetu tutaigawa katika Kanda nane, haya maeneo tungependa tuweze kufungua watu hata kutoka Nje waweze kupata huduma.Tumeishateua kamati ya watu ambao watasimamia jambo hili kwani ni lazima ziwe na ubora.Pia tutakuwa katika eneo la uwekezaji kwa kuweka teknolojia ya hali ya juu na Taasisi zetu ziweze kuzalisha pamoja na mapato.
“Ningependa kuona tunazipanua hizi hospitali za Mikoa mwaka huu tungependa kufanya ndani ya bajeti yetu tungependa kuona miradi ambayo haijakamilika inakamilika kuna majengo zaidi ya 22 yanaendelea yapo zaidi ya 180 ambao mpo katika hayo maeneo simamieni hiyo miradi inakamlika hela zipo.
“Mapato wekeni utaratibu mzuri ili Hospitali yako iwe vizuri ikiwezekana utumie hata kwenye miradi mingine,”amesema.
Naye,Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia magonjwa yasiyoyakuambukiza kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali,Dkt.James Kihologwe amewataka waganga hao kupeleka mipango mikakati yao Wizarani kwa kuangalia mazingira ya sasa ya ugonjwa wa Uviko 19 ambao umekuwa ukileta changamoto kadhaa pamoja na suala la maadili kwa wafanyakazi.
“Hivi karibuni yamejitokeza matukio mengi ya matukio ya watoa huduma kufanya mambo ambayo sio mazuri nanyi katika maeneo yenu ya kazi mna mabaraza kuhakikisha yanafanya kazi yake vizuri kwahiyo mwende mkasimamie haya kuhakikisha maadili ya watoa huduma yanaimarishwa na kuwachambua kuona wale wenye changamoto za maadili pelekeni katika mabaraza ili wachukue hatua,”amesema