******************************
Na Sixmund J. Begashe
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maonesho ya Sanaa na wasanii (Museum Art Explosion) ya kila mwezi yanayo ratibiwa na Makumbusho ya Taifa kupitia kituo chake cha Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Bw Mawazo Ramadhani alipokuwa akikaguwa hatua za mwisho za uwekaji Maonesho hayo ambayo yanatarajiwa kuhudhuriwa wa watu mbalimbali wakiwemo viongozi na wataalamu wa Makumbusho kutoka nchi ya Malawi.
Bw Ramadhan amesema tofauti na maonesho mengine ni kuwa, maonesho ya mwezi huu yametoa fursa kwa wasanii wakongwe nchini ambao wameipatia sifa Tanzania kitaifa na kimataifa kupitia kazi zao za sanaa lakini pia program hii imekuwa gumzo kwenye nchi za nje ndio maana wataalam wa kimakumbusho kutoka nchini Malawi wamekuja kuhudhuria.
“Makumbusho ya Taifa nchini imekuwa ni mfano wa kuigwa na nchi nyingi barani Afrika na nje ya Afrika hasa kwa namna ya uongozi wake, shughuli zake za utafiti, ukusanyaji, uhifadhi, uoneshaji wa urithi wa Utamaduni na wa Malikale pamoja na namna inavyo jiweka karibu na jamii kupitia program mbalimbali, ndiyo maana wenzetu wa Malawi wameona waje kujifunza kutoka kwetu.” Alisema Bw Ramadhani
Mkuu wa Idara ya Program, Bw Chance Ezekiel ameelaza kuwa, wamemwalika Mkuu wa Mkoa, kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ni kitovu cha wasanii mbalimbali hapa nchini ambao wamekuwa wakifanya kazi zinazo sambaa ndani na nje ya nchi hivyo, ni wakati muafaka kwa yeye kukutana na kuona kazi za wasanii hao waliovuma tangu miaka ya 80.
“Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni ipo Dar es Salaam, na ndio inayoendesha hii program ya MAE, wasanii hawa na adhira yao ni wakazi wa hapa, hivyo ni vyema mwenye Mkoa wake akaona kazi nzuri wanazofanya wasanii hawa ambao huwa awapewi nafasi kubwa na vyombo vya habari ukilinganisha na wale wa kizazi kipya” Aliongeza Bw Ezekiel
Licha ya kuushukuru uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kuona umuhimu wa kutoa nafasi kwa wasanii wakongwe nchini kuonesha kazi zao, Bw Raza Mohamed ametoa wito kwa watanzania kuja kwenye maonesho hayo ili wapate nafasi ya kujifunza na kuburudika lakini pia wasanii chipukizi kupata nafasi ya kuona ubora wa kazi za Sanaa na kujifunza kutoka kwa wakongwe hao.
Maonesho ya Museum Art Explosion ufanyika kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi kwa kutoa nafasi kwa wasanii watanzania kuonesha kazi zao za Sanaa za ufundi na za jukwaani ambapo kwa mwezi huu tarehe 24 Septemba saa 12 jioni wasanii wakongwe wataonesha kazi zao za Sanaa za ufundi huku Tanzania Philomeonic Society watafanya onesho la Muziki (CLASSICAL MUSIC)