Mkuu wa Wilaya ya Busega ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Busega, amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaojihusisha na uhalifu, ambapo siku za hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya uhalifu ikiwemo wizi katika maeneo mbalimbali Wilayani Busega. Mhe. Zakaria ameyasema hayo wakati alipofanya mkutano wa hadhara kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Nyashimo, tarehe 22 Septemba 2021.
Wakitoa kero zao wakazi wa Kata hiyo wanasema kwamba, hali ya uhalifu imekuwa ikiongezeka na kueleza kwamba hali hiyo imekuwa ikileta taharuki kubwa kwa wakazi wa Kata hiyo na Wilaya kwa ujumla. Wanaeleza kwamba kumekuwa na vikundi vinavyojihusisha na wizi wa kupora na kuvunja nyumba na kuiba mali mbalimbali ikiwemo fedha na vitu vingenevyo.
“Ni kweli nimepata malalamiko za uhalifu hasa wa uporaji, lakini nataka kusema watu wasijaribu kufanya uhalifu, mimi na vyombo vyangu vya ulinzi tupo macho na tunaendelea kuwabaini wote ambao wanajihusisha na uhalifu, ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi yao”, aliongeza Mhe. Zakaria.
Wananchi wa Kata hiyo wameomba Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuchuku hatua za haraka ili kuhakikisha uhalifu ambao umeanza kushamiri maeneo mablimbali Wilayani Busega unakomeshwa kwa kuwashughulikia wote wanaojihusisha na matukio hayo.
Pamoja na mambo mengineyo, wananchi wa Kata ya Nyashimo wameweza kueleza kero mbalimbali ikiwemo changamoto ya mioundombinu ya barabara za vijiji, uwepo wa soko la Wilaya, na eneo la makaburi ya Wilaya, huku ufafanuzi wa kina ukitolewa juu ya kero hizo. Mhe. Gabriel Zakaria anaendelea kusikiliza kero za wananchi maeneo mbalimbali za Wilaya ya Busega, ikiwa ni utaratibu aliojiwekea.