Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Mchungaji Dk. Mecka Ogunde,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa hilo yanayotarajia kufanyika September 27,2021 jijini Dodoma.
……………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Mchungaji Dk. Mecka Ogunde amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 50, ya Kanisa hilo yatakayofanyika Septemba 27, mwaka huu Jijini Dodoma.
Hayo ameyasema jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa Maadhimisho hayo yatahudhuriwa na wachungaji zaidi ya 2,000.
Dk. Ogunde amesema kuwa kanisa hilo mwaka huu linatimiza miaka 50 tangu kusajiliwa rasmi nchini kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“Kanisa letu mwaka huu linafikisha miaka 50, tangu kusajiliwa rasmi na sheria zetu za nchi na tumepanga Jumapili ijayo ya Septemba 26, tutafanya ibada ya maadhimisho haya itakayoongozwa na Askofu Mkuu Maimbo Mndolwa,”amesema
Pia amesema kuwa Rais Samia atahutubia wachungaji zaidi ya 2,000 watakaoshiriki katika maadhimisho hayo ambapo pia kutakuwa na wawakilishi wa makundi mbalimbali.
“Wachungaji hawa zaidi ya 2,000 wataanza kuingia leo jijini hapa kwani kabla ya maadhimisho haya kutakuwepo na kongamano litakalo wajumuisha wachungaji wote wa Kanisa la Anglikana Tanzania,”amesema Dk. Ogunde.
Aidha ameelezea mafanikio ya kanisa hilo kwa miaka 50, alisema limekuwa na mchango mkuwa kwa taifa hasa katika masuala ya afya na elimu.
Dk. Ogunde amesema kanisa hilo lilikuwa la kwanza kuanzisha kituo cha afya katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
“Kama nilivyosema kanisa hili ndiyo lilikuwa la kwanza kuanzia huduma za matibabu lakini pia tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi namna ya kujilinda na magonjwa mbalimbali ikiwemo UVIKO-19 ambapo tumetoa barakoa, vitakasa mikono na ndoo za kunawia mikono,”amesema Dk. Ogunde.
Amefafanua kuwa katika sekta ya elimu kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele kuanzisha shule kuanzia ngazi ya awali hadi vyuo vya kati na vyuo vikuu.
Vilevile, amesema kuwa kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa ukeketaji kwa mabinti.
“Tumeanzisha vituo vya kuhifadhi watoto waliokimbia vitendo vya ukeketaji ambavyo vinawahifadhi kwa kuwapatia elimu pamoja na ulinzi katika mikoa ya Mara, Arusha, Manyara pamoja na Dodoma,”ameelezea