***************************************
Na. Angela Msimbira MOROGORO
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa a Serikali za Mitaa Mhe Ummy Mwalimu amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya elimu kwa kujenga madarasa manne yenye thamani ya shilingi milioni 80 katika shule ya sekondari ya Matombo, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mkoani Morogoro
Akikagua miradi ya maendeleo leo katika Halmashauri hiyo Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya elimu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia
Akikagua ujenzi wa maabara ya shule ya Sekondari
Matombo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Waziri Ummy amesema Serikali itajenga bweni kwa ajili ya shule hiyo ili kupunguza adha kwa wanafunzi wanatembea umbali mrefu kufuata elimu
Waziri Ummy amesema ameridhishwa na Ujenzi wa maabara katika shule ya Sekondari ya Matombo iliyojarimu kiasi cha shilingi milioni 30 hali ambayo itasaidia wanafunzi wa masomo ya sayansi kusoma kwa vitendo.
Amesema kuwa kazi itaendelea chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassani kwa viwango vya hali ya juu, kasi na matarajio yaleyale yaliyokuwepo katika awamu ya tano
Akiongea kuhusu elimu bila malipo Waziri Ummy amesema kumekuwepo na uvumi kuwa elimu bila malipo haitaendelea suala hilo ni uongo na kusema kuwa katika kudhibitisha hilo tayari Mkoa wa Morogoro imepokea kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya elimu bila malipo na kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro wamepokea shilingi milioni 214 kuanzia julai hadi Septemba 2021 kwa ajili ya elimu bila malipo
Aidha amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa na nyumba za waalimu nchini