Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo akiongea na watumishi wa Chuo cha Ualimu Mpuguso (hawapo pichani) wakati alipotembelea kukagua miundombinu ya chuo hicho kilichopo Tukuyu mkoani Mbeya.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Mpuguso cha Tukuyu mkoani Mbeya wakiwa katika moja ya madarasa mapya yaliyojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Mradi wa UTC.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo akikagua moja ya mabweni yaliyopo Chuo cha Ualimu Mpuguso wakati alipotembelea kukagua miundombinu ya chuo hicho kilichopo Tukuyu mkoani Mbeya.
Muonekano wa mojawapo ya maabara ya iliyopo Chuo cha Ualimu Mpuguso, Tukuyu mkoani Mbeya
Muonekano wa maghorofa ya nyumba za wakufunzi zilizopo Chuo cha Ualimu Mpuguso, Tukuyu mkoani Mbeya
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Ualimu Mpuguso na wa Wizara hiyo wakati alipotembelea kukagua miundombinu ya chuo hicho kilichopo Tukuyu mkoani Mbeya.
…………………………………………..
Na WyEST,Tukuyu
Wakufunzi wa Vyuo vya Ualimu vya umma wametakiwa kutumia TEHAMA katika ufundishaji ili kwendana na ukuaji wa teknolojia duniani.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Mbeya na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo wakati alipotembelea Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo Tukuyu mkoani humo.
Amesema ni muhimu kwa wakufunzi kwendana na ukuaji wa teknolojia kwa kuwa shule nyingi sasa hivi zina maktaba mtandao na vifaa vya kidigitali hivyo ni vema walimu tarajali wakatoka chuo wakiwa na ujuzi watakaoutumia kwa wanafunzi wao.
“Tunatambua wakufunzi mmepewa mafunzo ya Tehama na hapa mna facilities zote za Tehama. Vyuo vya ualimu sasa vimekuwa vya kidigitali kwa hiyo hayo mafunzo mliyopata yatumike madarasani ili walimu tarajali wakitoka hapa nao wakayatumie kufundishia,” amesema Prof. Nombo.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo ameutaka Uongozi wa chuo kwa kushirikiana na wanafunzi kuhakikisha wanatunza miundombinu ya chuo ili iweze kutumika kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.
“Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 10.2 katika miundombinu ya chuo hiki ili Watanzania wengi waje kusoma hapa, hivyo tunatarajia miundombinu hii mtaitunza ili iweze kutumika na kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Prof. Nombo
Akitoa taarifa ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo, Stephen Mgimba amesema chuo hicho kinatoa mafunzo ya ualimu wa elimu ya msingi, elimu ya awali na Stashahada ya elimu ya ualimu wa Sekondari na kwamba kina jumla ya wanafunzi 554.
Mgimba amesema chuo hicho pia kina miradi mbalimbali ambayo mapato yake yanasaidia kutatua changamoto mbalimbali kama ukarabati mdogo wa miundombinu na kulipa mishahara wafanyakazi wa mikataba. Ametaja miradi hiyo kuwa ni mashamba ya chai, kahawa, migomba, miti na maparachichi. Pia kuna mradi wa duka na ukodishaji wa ukumbi.
Aidha Mwalimu Mgimba amemuahidi Naibu Katibu Mkuu huyo kutekeleza maagizo yote aliyotoa ikiwemo kuitunza miundombinu ili iweze kutumiwa na kizazi cha sasa na baadaye.