Muonekano wa tangi la Maji katika Mradi wa Maji Kemondo wilayani Bukoba , Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua tangi la maji katika Mradi wa Maji wa Kemondo wilayani Kigoma, Septemba 20, 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada kukagua Mradi wa Maji Kemondo wilayani Bukoba, Septemba 21, 2021. Wa pili kushoto ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa, kushoto ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza na wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Joseph Mbuge.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
.…………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameweka mikakati madhubuti unayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vyote nchini vikiwemo vya wilaya ya Bukoba mkoni Kagera.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza kampeni ya Rais Mheshimiwa Samia ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana karibu na kuwawezesha wanawake na vijana katika maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini kupata muda wa kushiriki katika shughuli za kijamii.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 21, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika kata ya Kemondo baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa Kemondo-Maruku akiwa katika katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti yenye lengo la kumaliza tatizo la maji nchini, hivyo wananchi waendelee kuwa na subra kwani mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa viwango ili wapate huduma hiyo kama ilivyokusudiwa.
Awali, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Bukoba, Mhandisi Evaristo Mgaya alisema mradi huo unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika kata tano za wilaya ya Bukoba na moja ya wilaya ya Muleba.
Mhandisi Mgaya alisema mradi huo unaotekelezwa kwa awamu na ya kwanza itahusisha kata mbili za Kemondo na Maruku kwa gharama ya shilingi bilioni 6.8, ambapo alitaja baadhi ya kazi zinazoendelea kuwa ni pamoja na ujenzi wa tanki la lita milioni tatu, uchimbaji wa mitalo ya kulazia mabomba ya kusambazia maji.
“Mradi huu umelenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika vijiji vya kata za Kemondo, Maruku, Nyangereko, Bujugo na Katerero wilayani Bukoba na kata ya Muhutwe wilayani Muleba. Mradi huu unatekelezwa kwa awamu na umekadiriwa kunufaisha wananchi 117,461 kwa gharama ya shilingi bilioni 15.9.”
Baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji, Waziri Mkuu alikagua mradi mwingine wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Bukoba inayojengwa katika kata ya Bujunangoma, ambapo aliwaagiza viongozi wa mkoa wa Kagera na Wilaya ya Bukoba wahakikishe wanasimamia kwa karibu miradi hiyo.
“Mkuu wa Mkoa (Meja Jenerali Charles Mbuge) na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba (Moses Machali) simamieni na fuatilieni miradi yote, majengo yajengwe kwa kuzingatia viwango. Mkuu wa mkoa hakikisha unachukua hatua kali kwa maafisa manunuzi watakaobainika kununua vifaa vilivyo chini ya kiwango.”
Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa wilaya ya Bukoba, ujenzi wa hospitali hiyo unafanyika kwa awamu ambapo amwamu ya kwanza ilihusisha majengo saba ambayo ni la wagonjwa wa nje, maabara, mama na mtoto, mionzi, utawala, kufulia pamoja na la kuhifadhia dawa. Ujenzi huo umegharimu shilingi bilioni 1.8.
Alisema awamu ya pili ya ujenzi huo ambayo inaendelea inahusisha ujenzi wa majengo ya wodi tatu ambayo ni jengo la wodi ya watoto, jengo la wodi ya wanaume na jengo la wodi ya wanawake. Ujenzi huo upo katika hatua ya upauaji. Ujenzi huo utakapokamilika utagharimu shilingi milioni 500.