Na Joseph Lyimo
UKATILI wa kijinsia unakinzana na haki za binadamu, utu wa mtu unapashwa kudhamini kwani kila mtu ni sawa chini ya sheria haijalishi ni mwanaume, mwanamke au mtoto.
Matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Manyara, yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwa vyombo vya habari kuripoti ikiwemo vipigo kwa wanawake na watoto hadi kusababisha majeruha au vifo.
Jeshi la polisi mkoani Manyara, kupitia dawati la jinsia wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii kutochukua sheria mkononi na kushirikisha vyombo vya sheria lakini suala hilo llimekuwa bado halijawaingia watu ipasavyo kwani matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto bado yanaripotiwa kutokea.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, kamishna msaidizi (ACP) Merrison Mwakyoma amesema matukio ya ukatili wa kijinsia yamekuwa yakitokea mara kwa mara japokuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii ili kukomesha hayo.
Kamanda Mwakyoma amesema hivi karibuni kulitokea matukio zaidi ya 10 ya ukiukwaji wa haki za binadamu ambapo wanawake na watoto walifanyiwa na watuhumiwa wanashikiliwa polisi au kufikisha mahakamani.
Ametaja baadhi ya matukio hayo ni Agosti 19 mwaka huu kwenye mtaa wa Silaloda mjini Mbulu, Harold Hhando (35) alimuua mtoto wa kike wa kaka yake Emmanuela Hhando (13) na kumpasua katikati ya miguu na kumtenganisha vipande viwili na kutoa maini ili ayapike.
Amesema Agosti 23 mwaka huu mkazi wa kijiji cha Kiongozi wilayani Babati Lucas Mangu (46) alimuua kwa kipigo mke wake Anna Kisino (41) kwa wivu wa kimapenzi hata hivyo naye Mangu alijinyonga.
“Tukio lingine la ukatili kwa mtoto lilitokea Septemba 12 mwaka huu mjini Babati ambapo Janeth Vicent alimchoma moto sehemu mbalimbali za mwili motto wake wa miaka mitatu baada ya kumuomba fedha mpita njia,” amesema kamanda Mwakyoma.
Amesema Septemba 4 mwaka huu kinyozi wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, Athuman Rajabu (57) alimlawiti mvulana mwenye umri wa mika 16 ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuzungumza.
Mkazi wa Dagailoi mjini Babati, John Paulo amesema matukio ya wanaume kupiga au kuwaua wanawake kutokana na wivu wa kimapenzi yamekuwa yakijirudia mara kwa mara.
Paulo amesema ni bora kumuacha mwanamke kuliko kumpiga au kumsababishia kifo kwa wivu wa mapenzi ambayo mara nyingi inakuwa hakuna uhalisia ni kuhisi tuu na kuchukua hatua kali.
Mratibu wa chama cha wanasheria wanawake Tanzania (TAWLA) kanda ya kaskazini, mwanasheria Happiness Mfinanga amesema jamii haipaswi kufumbia macho ukatili ila wanapaswa kutoa taarifa kwa vyombo husika.
“Jamii ipaze sauti kwenye hilo kwani kuna vyombo vya kisheria ambavyo vinawaelekeza kutoa ushauri ili kuepuka madhara zaidi ya ukatili majumbani mwetu,” amesema Mfinanga.
Amesema vipo vyombo vya kutoa taarifa ikiwemo dawati la jinsia ili kuepusha matukio ya kikatili yanayotokea kwa jamii siyo ya kufumbia macho na ushirikiano uanze kwenye familia hadi serikalini.
Mwandishi wa habari mwandamizi Peter Saramba anasema kwa mtazamo wake, tatizo la mwanaume kumuua mwanamke kutokana na wivu wa mapenzi ni ukatili wa mmomonyoķo wa maadili kuanzia kwenye kuanzisha mahusiano na hata kuishi kwenye mahusiano yenyewe.
Saramba anaeleza kuwa watu wanaingia kwenye mahusiano na hata kufikia hatua ya ndoa bila kila mmoja kumfahamu vema mwenzake na baadhi ya walioko kwenye mahusiano wanataka waendelee kuishi maisha yao ya mwanzo kabla ya uhusiano.
“Jambo ambalo kiuhalisia haiwezekani kwa sababu mahusiano na ndoa ni jela ya hiari anakoingia mtu akifahamu vema kuwa anajifunga kwa mwingine, ni kwa sababu yeyote anayeingia jela lazima apoteze baadhi ya vitu au mambo anayoyapenda lakini hayaruhusiwi jela,” amesema.
Amesema watu wengi waliopo kwenye mahusiano na ndoa hawazungumzi kujadili na kutafutia ufumbuzi matatizo na changamoto zao na wanawake hutumia silaha na mbinu za kike, hivyo hivyo wanaume kwao pia.