Kocha msaidizi wa Klabu ya KMC FC, Habibu Kondo amesema kuwa tangu kuanza kwa maandalizi kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu soka Tanzania bara msimu wa 2021/2022 (Pre seasons) hadi sasa kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni kimekuwa na muendelezo mzuri na kwamba mikakati zaidi ya kukisuka kikosi hicho inaendelea.
Habibu amesema kuwa kwa kipindi cha majuma matatu tangu KMC FC ianze ndaalizi yake ,Timu inaendeleakujengeka vizuri na kwamba kinachoendelea kwa sasa ni kukisuka vizuri zaidi kabla ya kuanza kwa michezo ya Ligi Kuu soka Tanzania bara ambapo tayari Bodi ya Ligi imeshatoa ratiba ya kuanza kwa kipute hicho.
Amefafanua kuwa wachezaji wote wa klabu hiyo wapo vizuri kwenye mazoezi na kwamba maboresho mbalimbali yanaendelea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Timu inacheza mechi za kirafiki ambazo zitakuwa na uwiano sawia ikilinganishwa na zile ambazo zimechezwa hadi sasa.
“ Tumekuwa na wakati mzuri kwenye mazoezi katika kipindi hiki ambacho tunafanya maandalizi kuelekea katika michezo ya ligi kuu, wachezaji wapo vizuri na cha kuwapongeza zaidi wanaonesha nia ya kutaka Timu ifanye vizuri kwenye michezo ya Ligi kuu ambayo tayari ratiba imeshatoka ambapo kwa mujibu wa Bodi ya Ligi KMC FC itaanza ugenini dhidi ya Polisi Tanzania Septemba 29 mwaka huu katika uwanja wa ushirika mkoani Kilimanjaro“ amesema Kocha Habibu.
Kama kocha kwa kushirikiana na benchi nzima la ufundi kwa sasa tunaangalia namna yakupata mechi nyingine za kirafiki ambazo zitaendelea kutupa taswira halisi lakini pia kuwajenga wachezaji wetu, tumeshacheza mechi mbili na Timu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza na kwasasa tunapanga kucheza na Timu zinazoshiriki ligi kuu” ameongeza Kocha Habibu.
Hadi sasa KMC FC imeshacheza mechi mbili za kirafiki ambapo mchezo wa kwanza ilikuwa ni dhidi ya Fountain gate ,mchezo ambao ulipigwa mkoani Morogoro ambapo KMC FC ilipotez mchezo huo kwa kufungwa goli moja kwa sifuri huku mchezo wa pili ukihusisha Timu ya Dar City uliopigwa katika uwanja wa Sekondari ya Benjamini Mkapa na KMC FC kupata ushindi wa magoli mawili kwa sifuri.