Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kidenge, Kata ya Luhundwa, Jimboni kwake Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, leo, amesema ataendelea kukemea matumizi mabaya mitandao na hata ogopa vitisho vya mtu yeyote kwa kuwa ameapa kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, George Fwime (kushoto), akimwekea fimbo ya umoja na ushirikiano Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia) na Diwani wa Kata ya Luhundwa, Richard Maponda, katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Kidenge, katika Kata hiyo, Jimbo la Kibakwe, Wilayani Mpwapwa,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kushoto), akimsikiliza Diwani wa Kata Luhundwa, Richard Maponda, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kidenge, Kata hiyo, Jimboni kwake Kibakwe, Wilayani Mpwapwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene (kulia), akipokea fimbo ya uchifu kutoka Anitha Magowa kwa mwakilishi wa wananchi wa Kijiji cha Kidenge, Kata ya Luhundwa, Jimboni kwake Kibakwe, leo, katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata hiyo ambao umejadili masuala mbalimbali ya maendeleo jimboni humo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
…………………………………………………………………………..
Na Felix Mwagara, MoHA, Kibakwe.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema ataendelea kukemea matumizi mabaya mitandao na hata ogopa vitisho vya mtu yeyote kwa kuwa ameapa kupambana na uhalifu wa aina mbalimbali nchini.
Waziri Simbachawene amesema hayo baada ya baadhi ya watu wenye nia mbaya ya kupotosha kwa makusudi kauli yake aliyoitoa mwishoni mwa wiki kwa vyombo vya habari ya kukemea watu kufanya matumizi mabaya ya mitandao, wakidai kuwa Waziri huyo anaingilia uhuru wa vyombo vya habari na atafunga mitandao ya kijamii.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara na mamia ya Wananchi wa Kijiji cha Kidenge, Kata ya Luhundwa, Jimboni kwake Kibakwe, Wilayani Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, leo, Waziri Simbachawene amesema kauli hizo za wapotoshaji hao hazina ukweli wowote kwasababu yeye alizungumzia uhalifu wa mitandao na siyo vinginevyo.
“Ninaposimama kama Waziri niliyeapa kwa ajili hiyo, nasema tutumie mitandao hiyo vizuri, tutumie mawasiliano ya simu vizuri, tusiwaibie watu, wanaofanya hivyo wanafanya makosa, wachukuliwe hatua za kisheria, wanaotumia mitandao kutukana wenzao, kukashifu wenzao, kurusha picha za hovyo, wanafanya makosa maana jamii yetu imejengeka katika misingi, utaratibu na utamaduni wa kuheshimiana, eti naingilia uhuru wa vyombo vya habari, huko ndivyo wanavyojadili kwamba Simbachawene sasa naye atapoteza umaarufu kwasababu anaingilia uhuru wa vyombo habari,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, mitandao ya kijamii ni hatari kwa maendeleo ya nchi endapo itatumiwa vibaya, hatutaki kufika huko, sasa Serikali ipo macho na nimeshatoa maelekezo ya kupambana na wahalifu wote wanaotumia vibaya mitandao.
“Kuna rafiki yangu mmoja kanipigia simu kaniambia eti Simbachawene huko usiende sisi tunakutegemea sana, acha watu waseme, watu waseme wanawatukana wenzao?, watu waseme wanawaibia wenzao?, mimi nazungumzia uhalifu, sijazungumzia maendeleo ya sayansi na teknolojia, maendekeo ya mwasiliano yatabadilika, mikutano kwenye ‘twita’, kwenye ‘space conference’ itaendelea tu, lakini itumike kwa mujibu wa taratibu zilizopo na kwa staha na kuweka heshima ya kitanzania mbele,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, ni kosa kutumia mitandao ya kijamii kwa kuvunja sheria za nchi kwa kuwanyima watu wengine raha kwa kisingizio kwamba uhuru wa kutoa maoni, kila mtu anahitaji kuheshimiwa, sio unatukana, sio unakashifu, tena unaowakashifu ni viongozi, hata kama sio kiongozi mtu anastahili haki yake ya kuheshimiwa.
“Eti wanasema nitafunga ‘social media’ (mitamdao ya kijamii), mimi nimesema nitafunga ‘social media’? Mimi sijasema nitafunga ‘social media’, mimi nimesema tutumie kwa kuzingatia sheria, tusitumie kwa kuvunja sheria za nchi na kukashifu na kuwanyima watu wengine raha kwa kisingizio kwamba uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kutoa maoni upo, social media zipo, zitaendelea kuwepo lakini lazima tuzitumie kwa uangalifu kwasababu zinaweza kuvunja umoja na mshikamano wa kitaifa,” alisema Simbachawene.
Pia Waziri Simbachawene ameendelea kusisitiza kauli yake aliyoitoa wiki iliyopita ya kulitaka Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali wale wote wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya uhalifu ikiwemo kumkashifu na kumtukana Rais.
“Rais ni kiongozi wetu, amewekwa na Mungu, kumbeza kumtukana, kumkashifu, kumdhalilisha ni kosa, na unapomdhalilisha unalidhal;ilisha taifa, hao wanaofanya hivyo na pia hata kwa viongozi wengine wote tutawashughulikia,” alisema Simbachawene.
Aidha, Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo hilo, amesema Rais Samia kwa kipindi cha miaka miezi mitano ametoa bilioni mbili ambazo zimetolewa kwa ajili ya kurekebisha barabara za Jimbo hilo, ambapo kati ya fedha hizo, milion 500 zimetengwa kwa ajili ya kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.3 Kibakwe mjini.
Ameongeza kuwa, Rais Samia pia ametoa zaidi ya milioni 260 wa ajili ya maendeleo ya miradi mbalimbali katika Kata ya Luhundwa,
“Fedha hizo bilioni mbili za barabara tayari tumezigawa katika mchanganuo na tutakwenda kuzirekebisha barabara zetu pamoja na maeneo ambayo hatujayafungua tutayafungua, na pia Rais Samia tayari ameondoa shida ya maji katika Kata hii na sasa hakuna shida ya maji wala umeme, na pia ametoa zaidi milioni 260 ajili ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya Kata hii ya Luhundwa,” alisema Simbachawene.
Simbachawene anaendelea na ziara jimboni kwake kwa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.
MWISHO/-