Na Joseph Lyimo
WAANDISHI wa habari ni kundi la watu ambao wanafanya kazi zao kwenye jamii mbalimbali hivyo ni miongoni mwa wenye kuwa katika hatari ya kupata janga la UVIKO-19 endapo wasipochukua tahadhari.
Japokuwa tangu kuingia ugonjwa huo nchini Machi mwaka 2020 hakuna taarifa kamili ya waandishi wa habari walioripotiwa rasmi kufa kwa UVIKO-19 lakini hiyo haisababishi wao kutopata chanjo.
Mara nyingi waandishi wa habari huwa wanaandika changamoto za kada za watu wengine au kuandika watu wa sekta au jamii nyingine zikapate chanjo ila wao wanakuwa na mwitikio mdogo utadhani hawahusiki.
Mwandishi wa habari wa mjini Babati mkoani Manyara, Mariam Juma amesema ameshapata elimu juu ya chanjo inayotolewa na anatarajia kupata chanjo kwenye hospitali ya Mrara.
“Tumepewa elimu kuwa chanjo ni nzuri haina tatizo lolote hivyo nipo tayari kwenda kupatiwa chanjo kwani siyo vizuri sisi waandishi wa habari kuandika habari za chanjo huku bado hatujachanja,” amesema Mariam.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Manyara (MAMEC) Mary Margwe, amesema yeye ameshapatiwa chanjo hiyo mjini Mbulu tangu Agosti 10 mwaka huu.
Margwe amesema wataalamu wa afya na serikali kwa ujumla wamekuwa wakitoa elimu ya chanjo hiyo kuwa haina tatizo lolote hivyo waandishi wa habari nao wanapaswa kuchanja.
“Waandishi wa habari tuonyeshe mfano kwa kuhakikisha tunapatiwa chanjo kwani wataalamu wanasema japokuwa haizuii kupata maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 lakini matarajio ya kupona ni makubwa tofauti na mtu ambaye hana chanjo.
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari za jamii ya pembezoni (MAIPAC) Mussa Juma amesema waandishi wa habari wanapaswa kupata chanjo ili waweze kufanya kazi zao kwa usalama zaidi.
Mussa amesema yeye ameshapata chanjo ya UVIKO-19 hivyo ni vyema waandishi wengine zaidi wakachanje kwani mwitikio wao kwenye kuchanja ni mdogo kuliko matarajio ya wengi.
“Waandishi wa habari wanatakiwa kupata chanjo kwani wanaweza kukosa hata fursa ya kwenda nje ya nchi ghafla kutokana na kutopata chanjo ya UVIKO-19,” amesema Mussa.
Amesema waandishi wa habari wamekuwa wanaandika habari kwa kutoa elimu kwa wananchi wakapate chanjo lakini wao wenyewe wamekuwa na mwamko mdogo wa kuchanja.
“Pamoja na kuwa waandishi ni kundi lililopo hatarini kupata maambukizi ya UVIKO-19 lakini wamekuwa nyuma kutimiza suala zima la kuchanjwa ila muda bado upo wanaweza kuchanja,” amesema Mussa.
Hivi karibuni, mwandishi wa habari mkongwe Gasirigwa Sengiyumva ametoa mafunzo ya namna ya kuandika habari na kujikinga na UVIKO-19 kwa waandishi wa habari jijini Arusha, iliyowezeshwa na shirika la Journalist for Human Rights (JHR) na kuandaliwa na chama cha waandishi wa habari za jamii ya pembezoni, (MAIPAC).
Gasirigwa amewapa miongozo 17 waandishi hao wa habari za kujikinga na UVIKO-19 pindi wakiwa wanafanya shughuli zao za kuchakata, kuandika na kutangaza kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo magazeti, mitandao ya kijamii, redio na runinga.
Ametaja miongozo hiyo ni waandishi wa habari kujikinga ili wasipate UVIKO-19 kisha wakawa habari hivyo waandike habari zao na kujikinga wasiathirike.
Ametaja miongozo mingine ni kunawa mikono kwa maji tiririka, kuvaa barakoa, kuacha nafasi pindi wanapofanya mahojiano, kutakasa vipaza sauti na kuchukua tahadhari kwenye usafiri wa jamii.
“Mnapaswa kupata mlo kamili kwa kula chakula kuanzia asubuhi, mchana na jioni, kwani siyo vyema kufanya kazi ya uandishi wa habari tumbo likiwa halina chochote,” amesema Gasirigwa.
Amesema ni vyema waandishi wa habari wakafanya kazi nyumbani au ofisini kwao kama hakuna sababu ya kufika kwenye maeneo ya matukio na kufanya mahojiano.
“Fanyeni mahojiano kwa njia ya simu, mkitumia data na mtandao ili kufanikisha habari na siyo lazima ufike kwenye eneo la tukio kama hakuna ulazima,” amesema Garisigwa.
Amesema pia waandishi wa habari wanaochukua matukio ya picha au mahojiano wanapaswa kutumia vipaza sauti virefu vyenye kufika kwa muhojiwa bila kumsogelea.