Na Joseph Lyimo
JANGA la UVIKO-19 limekuja na changamoto kubwa kwa jamii ya wafugaji wa kimasai kwa utaratibu wa namna wanavyosalimiana kwa kushikana mikono na kushikwa kichwa bila kuchukua tahadhari za UVIKO-19.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kusogeleana na kugusana ni miongoni mwa visababishi vya kuambukizana ugonjwa wa UVIKO-19 endapo mmoja kati ya mtu atakuwa na maambukizi hayo.
Mtoto wa jamii ya kifugaji wa kimasai akimkuta mzee au mtu aliyemzidi umri inamlazimu kumsalimia kwa kumwinamia na kumpa kichwa ili ashikwe kichwani katika kuonyesha heshima.
Pia, kwenye jamii hiyo watu waliopo kwenye umri uliokaribiana au waliolingana ni wajibu kushika mikono katika kusalimina kwao.
Mkazi wa mji mdogo wa Orkesumet, John Mollel anasema salamu za jamii hizo zimekuwa na changamoto kubwa kwao kutokana na kipindi hiki cha uwepo wa ugonjwa wa UVIKO-19.
Amesema inaonekana ni utovu wa nidhamu usipofuata mila na desrtu kwani kijana ataonekana anakinzana na mila na desturi zao hivyo ni lazima aumpe kichwa au mkono japokuwa wataalamu wa afya wamejitahidi kutoa elimu kwa kipindi hiki.
Ofisa tarafa ya Moipo Joseph Mtataiko anasema ni vigumu kwa jamii ya kifugaji wa kimasai kutosalimiana kwa kushikana mikono au kushikwa kichwa kwa hofu ya kuambukizana UVIKO-19.
Mtataiko amesema japokuwa wengine kwenye jamii hiyo wameelimika baada ya kupatiwa elimu ya kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 lakini kwa wengine inakuwa kikwazo.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Purana, Enock Paulo anasema ugonjwa wa UVICO-19 pamoja na mambo mengine umekuja na changamoto ya salamu hiyo kwa wafugaji.
Mchungaji Paulo amesema ni mila na desturi kwa jamii ya wafugaji kusalimiana kwa kushikana mikono na wakubwa kuwashika kichwa wadogo na usipofanya hivyo inakuwa kosa.
“Hata hivyo jamii hiyo hivi sasa imebadilika kwa kuchukua tahadhari ya kusalimiana baada ya wataalam wa afya kutoa elimu ya afya ya tahadhari za UVIKO-19,” amesema mchungaji Paulo.
Diwani wa kata ya Shambarai, Julius Mamasita amesema ni jadi kwa jamii ya wafugaji wa kimasai kusalimiana kwa mkubwa kumshika kichwa mdogo na kusalimia kwa mkono.
Hata hivyo, Mamasita amesema hivi sasa jamii hiyo imepewa elimu ya kusalimiana kwa ishara ya kupungiana au heshima ya shikamoo kwa lugha yao na kupunguza ile ya mila na desturi zao.
Amesema salamu ya mdogo kushikwa kichwa na mkubwa kwa mila na desturi za kimasai ni kuonyesha unyenyekevu na heshima kwa mtu mkubwa aliyekuzidi umri.
kwa ya kichwa na mikono katika kkuchukua tahadhari hshima unyenyekevu kwa jamii ya kimasai
“Viongozi wa kimila (malaigwani) walielezwa na wataalamu wa afya nao wakawaeleza vijana kuwa hawawezi kusalimiwa bila kushikwa kichwa au kupeana mikopo sababu ya UVIKO-19,” amesema Mamasita.
Kiongozi wa kimila wa jamii hiyo Lazaro Lomoni, amesema japokuwa hakuna kikao kiliamua suala la salamu ya kupeana mikono na kusalimiana kwa mdogo kushikwa kichwa ila hivi sasa imepungua.
“Watu wanachukua tahadhari ya UVIKO-19 lakini pia wamtegemea Mungu moto kubanana kwenye viti,” amesema laigwanani Lomoni.
Kiongozi mwingine wa kimila wa laigwanani Lembris Makau amesema hofu ya kuchapwa viboko 70 kwa vijana nayo iliwapa hofu vijana wa jamii hiyo hivyo kuendelea na salamu za kawaida.
Amesema kwenye jamii hiyo kuna utaratibu wa kijana mmoja akikosea anachapwa viboko 70 na hiyo inaendana na rika lote Tanzania mtu akikosea Simanjiro hata kijana wa Monduli anachapwa.
Amesema utaratibu wa salamu uliendelea kama kawaida kwao kwani dawa ya sokonoi inaaminika kwa dhati kwani hata kama koromeo imezika ukipewa robo kikombe mapafu yote yanaachia.