Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kamal Group, Bw. Sameer Gupta akizungumza katika hafla ya utoaji wa miguu bandia kwa watu wenye uhitaji iliyofanyika Kerege, Bagamoyo mwishoni mwa wiki. katikati ni meneja rasilimali watu wa kampuni hiyo Bi. Emma Mwenda na kulia ni mjumbe wa bodi ya Kamal Group na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru. PICHA|MPIGAPICHA WETU
……………………………………………………………………………….
Watu 100 wenye ulemavu wameanza kutembea tena baada ya Kampuni ya Kamal ya Jijini Dar es Salaam kuwapatia miguu bandia.
Miguu bandia ipatayo 77 ilikabidhiwa kwa baadhi ya wanufaika katika hafla iliyofanyika katika eneo maalumu la viwanda linalomilikiwa na kampuni ya Kamal eneo la Kerege, Bagamoyo Mkoani Pwani mwishoni mwa wiki.
Hadi hivi sasa, Kampuni ya Kamal imetoa jumla ya miguu bandia 1000 kwa watu wenye ulemavu kutoka katika mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi miguu hiyo bandia kwa wanufaika, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge aliwataka wakazi wa mkoa wa Pwani kutumia vizuri uwekezaji uliofanywa na wawekezaji mbalimbali mkoani humo.
Alisema Mkoa wa Pwani unao zaidi ya watu 130,000 wenye ulemavu ambao wanahitaji huduma ya miguu bandia.
Bw. Kunenge aliwaasa wakazi wa Mkoa wa Pwani kujenga utamaduni wa kupenda kufanya kazi badala ya kuwaachia watanzania wenzao wanaotoka mikoa mingine kuja kushika nafasi mbali mbalimbali za kazi katika viwanda vinavyowekeza katika mkoa huo uliyo jirani na Dar es Salaam.
“Naomba niwape ukweli. Vijana wengi wa Mkoa wa Pwani hawapendi kufanya kazi. Ninapata malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wawekezaji wanaohoji ni kwa nini watu wa Mkoa wa Pwani hupenda kutoa udhuru mara kwa mara wawapo kazini? Utasikia leo anaenda kuzika na kesho kuna ngoma. Lazima tubadilike,” alisema.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamruhusu kila raia kuishi sehemu yeyote nchini ili mradi asivunje sheria na kuwataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kutokuwa watazamaji wenzao wanapopambana kufanya kazi.
Alisema tayari kampuni ya Kamal inatekeleza mpango wa kuwawezesha wajasiriamali wa Watanzania kumiliki viwanda vidogo vidogo vya kubangua korosho ambapo kwa kuanzia, watu zaidi ya 100 watamiliki viwanda vivyo vinavyojengwa katika Eneo Maalum la Viwanda la Kamal linalopatikana Kerege, Bagamoyo.
“Itapendeza kama viwanda hivi vitamilikiwa kwa kiasi kikubwa na wakazi wa Mkoa wa Pwani. Ichangamkieni hii fursa,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Zainabu Issa alisema hivis sasa wilayani hapo kuna jumla ya viwanda 145 vyenye ukubwa tofauti tofauti na kusisitiza kuwa serikali itafanya kila lilalowezekana kuweka mazingira sawa kwa wawekezaji kufanya kazi bila vikwazo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kamal Group, Bw. Sameer Gupta, alisema kampuni yake hutoa msaada wa miguu bandia kupitia taasisi yake ya kuwawezesha watu, yaani, People’s Empowerment Foundation – PEF).
Alisema kwa kutoa miguu bandia, taasisi ya PEF huwasaidia watu wenye ulemavu ili waendelee kufanya majukumu yao ya kujipaitia riziki kama ilivyokuwa mwanzo kabla hawajapata ulemavu.
Kampuni ya Kamal inafanya biashara katika maeneo mbali mbali ila imejijengea jina kubwa katika sekta ya nondo.
Mbali na miguu bandia, kampuni hiyo pia inatoa chakula kwa zaidi ya wanafunzi 3,500 wanaosoma katika shule za msingi za Chanika, Dar es Salaam na Nzasa ya Bagamoyo kwa muda wa miaka saba hadi hivu sasa ambapo taarifa zinaonyesha utoro umepungua kwa kiasi kikubwa.