****************************
Na Joseph Lyimo
WACHIMBAJI wa madini ya Tanzanite na wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kupatiwa chanjo ya covid-19 na kuepuka na maneno potofu ya mitandaoni kuwa watageuka kuwa mazombi.
Mchimbaji wa madini ya Tanzanite Juma Seif amesema dhana potofu zinazotolewa na baadhi ya watu zinapaswa kubezwa kwani serikali haiwezi kuwaletea tatizo kwenye suala la afya ya watanzania.
“Tuondokane na dhana potofu zinazotolewa na watu wasio na uelewa juu ya chanjo na kuzusha kuwa mara baada ya kuchanjwa utageuka kuwa zombi au mtu wa kutisha,” amesema Juma.
Amesema amepata chanjo ya covid-19 kwenye kituo cha afya Mirerani Agosti 8 mwaka huu na hajapata kupata madhara yoyote baada ya zoezi hilo.
Amesema wadau wa madini wanatakiwa kupata chanjo ili hata ikitokea bahati mbaya anapata maambukizi ya corona hapati maumivu makubwa kwa sababu alishapatiwa chanjo.
Mjumbe wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, MAREMA Tawi la Mirerani, Japhary Matimbwa amesema wadau wa madini ya Tanzanite wanatakiwa kuchanja na kuachana hofu na dhana potofu.
Matimbwa amesema dhana kuwa Rais wa awamu ya tano wa Tanzania hayati John Pombe Magufuli aligoma chanjo kutumika hapa nchini siyo ya kweli kwani alitoa agizo uchunguzi ufanyike kwanza ndipo chanjo itumike.
Amesema mara nyingi watanzania huwa wanawalisha maneno marehemu ambayo hawapo hivyo haitakiwi kuzungumza maneno mengi zaidi ya kupata chanjo.
“Hili suala la kusema marehemu alisema hivi akasema vile huwa ni kisingizio tuu mbona marehemu wengine wanasema nikifa mke wangu asiolewe ila baada ya miezi sita anaolewa na wengine wanasema nikifa nyumba yangu msiuze na baada ya mwaka watoto wanauza na kugawana pesa,” amesema Matimbwa.
Ameongeza kuwa wadau wa madini wanatakiwa kupata chanjo japokuwa wengine wangeweza kukimbilia chanjo hiyo endapo wangeambiwa ni chanjo ya ukimwi.
“Waachane na maneno ya kwenye vijiwe, serikali haiwezi kuwaletea sumu na tumeshapewa maelezo na wataalamu kuwa chanjo hii ni nzuri na haina tatizo lolote nipo sawa baada ya chanjo,” amesema Matimbwa.
Amesema yeye amechanja Agosti 6 mwaka huu kwenye kituo cha afya Mirerani hivyo anawaasa wananchi wa eneo hilo wakapate chanjo ili kupambana na janga la corona.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mirerani Dkt Deogratius Mazengo amesema wakazi mbalimbali wa eneo hilo wamejitokeza kupata chanjo ya covid-19 katika kituo hicho.
Dkt Mazengo amesema kwenye wilaya ya Simanjiro kuna vituo vitatu vya kupatiwa chanjo vya Mirerani, Orkesumet na Naberera, hivyo wananchi washiriki zoezi hilo.
“Mwitikio wa watu ni mzuri na wengine wanatoka wilaya za jirani za Arumeru mkoani Arusha na Hai mkoani Kilimanjaro hivyo wananchi wa eneo hilo wafike kupata huduma hiyo,” amesema Dkt Mazengo.
Amesema chanjo hizo ni salama zimedhibitishwa na shirika la afya duniani WHO na serikali ya Tanzania imezipitisha rasmi kutumika kwake.
Amesema tangu wameanza kutoa chanjo hiyo hakuna mtu aliyepata madhara hivyo wananchi wajitokeze kupata chanjo hiyo ambayo ni salama na anawakaribisha sana.
Amesema chanjo hiyo inatolewa kwa watu wenye kuanzia umri wa miaka 18 na wanawake wajawazito wanapaswa kusubiri kwanza hadi wajifungue.
Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo, amewahamasisha wananchi wa eneo hilo kuchanja na kuondokana na dhana potofu kuwa.
“Tusiwe na maneno mengi ambayo siyo yakitaalamu ukiona hata Rais Samia Suluhu Hassan amechanja na kuzindua zoezi hili na hakuna kiongozi anaweza kuua watu wake,” amesema Kobelo.
Amesema hata Dkt Mwele Malecela ambaye ni mtaalamu wa afya aliyepo nje ya nchi, amekuwa akitoa elimu ya afya kuhusiana na chanjo na ameelimika juu ya chanjo hiyo hivyo wadau wa madini wakashiriki kuchanja.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni mjini Babati amesema wamepokea kiasi cha dozi 15,000 za chanjo za covid-19.
Makongoro amesema maeneo mbalimbali ya hospitali, vituo vya afya na zahanati, za wilaya tano za mkoa huo za Babati, Simanjiro, Mbulu, Hanang’ na Kiteto, zimepatiwa chanjo hizo.
“Wananchi wanatakiwa kushiriki kikamilifu kupata chanjo hizo kwani serikali imeshafanikisha kuzisambaza maeneo mbalimbali ya mkoa wetu,” amesema Makongoro.