Mkuu wa Mkoa wa Pwani akipanda mti eneo la Kamal Industrial Park ikiwa ni sehemu ya program ya kampuni hiyo ya kutunza Mazingira.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Mnufaika Jane Almas akiwa ameinua juu mguu bandia Mara baada ya kuupokea kutoka Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Aboubakar Kunenge ((wa nne toka kushoto).(picha na Mwamvua Mwinyi)
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi miguu bandia kwa walemavu katika eneo la uwekezaji la KAMAL Group, Kerege- Bagamoyo leo Septemba 18, 2021.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
*************************************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge ,amekabidhi msaada wa miguu bandia yenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 50 iliyotolewa na “KAMAL Group” kwa walemavu kutoka Chalinze, Bagamoyo na Dar es Salaam.
Akikabidhi miguu hiyo bandia, Kunenge amewapongeza walengwa waliopata msaada huo na kuwaasa kuitunza ili iwasaidie kutekeleza majukumu yao kwa urahisi.
Kunenge ameishukuru “KAMAL Group” kwa kutoa msaada huo kupitia mpango wa kuwezesha wananchi “Peoples empowerment foundation-PEF.
“Kazi hii mnayofanya ni njema sana, inayompendeza Mwenyezi Mungu na ni zaidi ya matarajio ya kawaida ya kibinadamu, ni kazi ambayo imewasaidia wahitaji katika mambo mengi ikiwemo kuwawezesha kutembea ili kujitafutia riziki zao.” Alisema Kunenge.
Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa mkoa ameiomba “KAMAL Group” kuendelea na huduma hiyo kwa kuwa wahitaji bado wapo akitolea mfano mkoa wa Pwani ambao amesema unakadiriwa kuwa na walemavu wa viungo 130 ambao hawajafikiwa na huduma hiyo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Sameer Gupts, katika taarifa yake alieleza kuwa wamekuwa wakitoa viungo bandia kwa miaka tisa mfululizo sambamba na kutoa chakula cha mchana kwa Shule mbili za Msingi za Kerege iliyopo Bagamoyo Mkoani Pwani na Nzasa ya Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na kushiriki katika Kampeni za upandaji wa miti kama jitihada za kutunza mazingira ikiwa ni wajibu wao wa kurudisha sehemu ya faida yao kuchangia maendeleo ya jamii zinazowazunguka.