*******************************
Na WAMJW- DSM
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameliagiza Baraza la Uuguzi na Ukunga kuwachukulia hatua Wauguzi na Wakunga wote wanaovunja Sheria, maadili, miongozo na miiko ya taaluma Yao bila kuwaonea.
Dkt. Gwajima ametoa agizo hilo mapema leo Septemba 18, 2021 wakati akizindua Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, tukio lililofanyika katika Ukumbi wa kituo hicho kilichopo Kibaha, Mkoani Pwani.
“Nitoe rai kwa Baraza msisite kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu na Sheria zinazowaongoza na kamwe msimuonee mtu, lakini kwa upande wa wakunga na Wauguzi mnaoongozwa na Baraza hili nawaomba sana kwamba msijenge utaratibu wa kukiuka maadili miongozo na kanuni.” Amesema Dkt. Gwajima.
Amesema, Baraza lina wajibu mkubwa wa kuhakikisha linalinda, kuimarisha na kuhifadhi Afya ya Jamii, Usalama na Ustawi kupitia usimamizi na udhibiti wa shughuli za mafunzo ya Uuguzi na Ukunga, huku akiweka wazi kuwa karibu asilimia 60% ya Watoa huduma za afya hapa nchini ni Wauguzi na Wakunga ukilinganisha na kada nyingine.
Aliendelea kusema kuwa, Bado taaluma hii inazo changamoto hasa katika upande wa utoaji huduma kwa wananchi, hali inayopelekea kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, hivyo kuliagiza Baraza hilo kusimamia vizuri utoaji huduma bora na salama kwa wananchi.
“Bado tunazo changamoto katika taaluma hii, hususani katika utoaji wa huduma ambako tunaendelea kupokea malalamiko mengi hutoka kwa jamii. Hivyo, Baraza hili linatakiwa kuhakikisha kuwa jamii yetu inapata huduma bora na salama.”Amesema.
Hata hivyo, ametoa rai kwa Baraza hilo kutimiza majukumu yake kwa weledi na uthabiti mkubwa bila ya hofu ya kuingiliwa katika maamuzi yao watayofanya kwa lengo la kuboresha Sekta ya Afya hususan kwenye eneo la Uuguzi na Ukunga nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah amempongeza Mhe. Waziri wa Afya kwa uteuzi makini wa Baraza la Uuguzi na Ukunga ambalo litakuwa chachu ya kuleta matokeo chanya kwenye usimamizi na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kufuata Sheria na Kanuni za Uuguzi na Ukunga nchini.
Aliendelea kwa kulipongeza Baraza lililomaliza muda wake kwa jitihada kubwa walizofanya katika kufanya maboresho ikiwemo kuanzisha mfumo wa kanzidata ambayo imewezesha kuanza kutoa huduma kwa njia ya mtandao, kupata idadi ya Wauguzi na Wakunga kwa urahisi na kuweza kuwahakiki kama wamesajiliwa na wana leseni hai ya kutoa huduma.
Hata hivyo, ametoa rai kwa Baraza jipya kushughulika na changamoto za Baraza hilo ikiwemo rasilimali fedha ili kuwasaidia kutekeleza majukumu ya Baraza hilo kwa ufanisi na weledi.
Naye, Mwenyekiti wa sasa wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Prof. Lilian Mselle Kwa niaba ya Baraza jipya ameahidi kutimiza majukumu yote ya Baraza kwa kasi na weledi mkubwa, huku akisisitiza Baraza hilo litaendelea kushirikiana na Wadau mbali mbali wa masuala ya Uuguzi na Ukunga ili kuikuza zaidi taaluma hiyo na kuzalisha wahitimu walio na vigezo vyote kulingana na taaluma hiyo.