Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa Singida Dkt.Binilith Mahenge amewaomba viongozi mbalimbali mkoani hapa kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kushiriki zoezi la majaribio la Sensa ya Watu na Makazi.
Dkt.Mahenge ametoa ombi hilo katika kitongoji cha Gajaroda kilichopo Kijiji cha Dominiki wilayani Mkalama alipofika kukagua zoezi hilo ambalo limeonesha kupata mafanikio makubwa kutokana na uhamasishaji uliofanyika.
” Kama uhamasishaji uliofanyika katika eneo ili na hakukuwa na changamoto yoyote kama walivyosema wataalamu wetu wanaofanya kazi hii Mkoa wa Singida utakuwa na nafasi kubwa ya kufanikisha sensa itakayofanyika mwakani “. alisema Mahenge.
Alisema kama katika eneo hilo la kijijini limefanikiwa kwa kiasi hicho anaamini kwa maeneo ya mjini itakuwa ni nafuu zaidi.
Alisema lengo kubwa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ni kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa;
Alisema taarifa za idadi ya watu zitakazopatikana katika sensa hiyo husaidia mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali;
Alisema Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum. Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.
Alisema takwimu hizi za msingi ndiyo zinazoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi maalum yenye uhitaji maalum kwa mfano, watu wenye ulemavu, wanawake, watoto, vijana na wazee hivyo kurahisisha uandaaji wa sera na mipango ya maendeleo kulingana na uhitaji na mazingira yaliyopo.
“Jambo ili la sensa ni la muhimu sana hivyo nawaomba wananchi ninao waongoza walipokee kwani ndio msingi wa maendeleo ” alisema Mahenge.
Kalani wa Sensa katika eneo hilo Elifrida Yunde alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni umbali wa kutoka kaya moja na nyingine hivyo hutumia muda mwingi wa kuzifikia na kuwa wananchi wamekuwa wakiwapa ushirikiano mkubwa licha ya kushindwa kujibu maswali mengine kwa ufasaha hasa yanayohusu umiliki wa mali kama mifugo na mashamba.
Mkuu wa wilaya hiyo Sophia Kizigo alisema changamoto kubwa inayowakabili wataalamu hao ni wingi wa kaya ambazo wanazipitia kwani awali zilidhaniwa ni chache lakini baada ya kufika eneo la tukio wamezikuta ni nyingi akitolea mfano wa kitongoji hicho ambacho walikisia kitakuwa na kaya 150 kumbe kina kaya 273 ambazo ni zaidi ya kijiji ambapo aliomba ifanyiwe kazi.
Meneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Naing’oya Kipuyo alisema zoezi hilo linakwenda vizuri licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo.
Msimamizi wa Sensa Mkoa wa Singida Profesa Mourice Mbago alisema changamoto kubwa ilikuwa ni usafiri wa kutoka eneo moja kwenda jingine ambayo imetatuliwa kwa msaada wa viongozi wa eneo hilo kwa kuwashirikisha wananchi wenye pikipiki ambao wamekuwa wakijitolea kuwapeleka wataalamu hao katika kaya mbalimbali kuendelea na kazi.
Mkazi wa Kitongoji hicho Lusia Samsoni alisema sensa hiyo ni nzuri kwani itasaidia kupanga mipango ya maendeleo kama ujenzi wa shule, zahanati, barabara na mambo mengine mengi.