Na Dotto Mwaibale
WANAMUZIKI mbalimbali kupitia Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO) jana Wamefanya ziara ya matendo ya huruma na Kuhamasisha shughuli za maendeleo ya jamii ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Muziki Duniani ambayo kitaifa kwa mara ya kwanza yataadhimishwa Jijini Arusha Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuanzia Septemba 24 hadi OKtoba 1 ambapo ndio itakuwa kilele chake.
Akizungumzia ziara hiyo Katibu Mkuu wa TAMUFO Stella Joel alisema katika ziara hiyo wanamuziki hao walitembelea Shule ya Sekondari ya Jangwani ya jijini Dar es Slaam ambapo waliweza kujumuika na kutoa zawadi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na baada ya hapo waliendelea na ziara hiyo ya uhamasishaji wa maendeleo kwenda maeneo mengine yakiwemo Makumbusho ya Taifa ya Jijini Dar es Salaam.
Joel alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi na wanamuziki wote kushiriki maadhimisho hayo kwa kujitokeza kwa wingi siku hizo za maadhimisho hayo kuelekea Oktoba 1, 2021 ambayo itakuwa ni kilele chake ambapo kutakuwa na mambo mengi na burudani kubwa ya muziki kutoka kada tofauti ya wanamuziki wakiwepo wa Bongo Fleva, Dansi, Zuku, Injili, ngoma za asili na mingine mingi.