Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Dunstan Kyobya akimuelezea jambo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Jengo la Hospitali ya Rufaa Kandaa ya Kusini unaotekelezwa na NHC
Mshauri Mwelekezi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi Bw. Anania Saudeni akielezea maeneo mbalimbali ya Hopsitali ya Rufaa Kanda ya Kusini kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Ndugu Shaka Hamdu Shaka alipotembelea Hospitali hiyo leo.
Meneja NHC Mtwara Bi. Angela Magazi akisoma taarifa ya mradi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Ndugu Shaka Hamdu Shaka (hayupo pichani) alipotembelea mradi huo leo.
Hali ya Jengo la Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini Mtwara linalojengwa na NHC ilivyo hivi sasa.
*******************************
Na Mwandishi Wetu, MTWARA
Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Shaka Hamdu Shaka ametembelea mradi ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini Mtwara na kulipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri ya ujenzi wa jengo hilo la kisasa.
Akiwa katika ziara hiyo leo tarehe 17 Sept 2021, Shaka amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kinatambua kazi nzuri inayofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala.
‘’Kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi nalipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri ya kupigiwa mfano ya ujenzi wa jengo hilo la kisasa litakalosaidia kupunguza gharama kwa Wananchi wa Kanda ya Kusini za kufuata huduma ya matibabu ya ngazi ya rufaa Jijini Dar es salaam’’ alisema Shaka.
Amesema kuwa, kwa miaka mitano iliyopita NHC imekuwa ni kimbilio kubwa la Chama cha Mapinduzi katika utekelezaji mahiri na makini wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuliunga mkono Shirika hilo ili liweze kusaidia Watanania wengi zaidi.
Hata hivyo, Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi hakufurahishwa na maandalizi ya kuanza utoaji wa huduma kwenye Hospitali hiyo iliyokamilika kwa asilimia 97 kama Wizara ya Afya ilivyomuahidi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipofika kuweka jiwe la msingi la Hospitali hiyo Julai 26, 2021. Wizara hiyo kupitia Naibu Waziri wake Dkt. Godwin Mollel ilimhakikishia Makamu wa Rais kuwa Hospitali hiyo ingeanza kutoa huduma mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2021.
Kufuatia hali hiyo, Ndugu Shaka ameiagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuacha urasimu na kuhakikisha inatekeleza ahadi yake ya kuanza kutoa huduma katika Hospitali hiyo ifikapo Oktoba 2021.
”Sioni dalili yoyote ya kuanza utoaji wa huduma hapa, hakuna vifaa wala maandalizi ya muhimu ya kuanza utoaji huduma” alisisitiza Ndugu Shaka kwa masikitiko makubwa.
Mapema akiongea baada ya ukaguzi wa jengo hilo kubwa la kisasa, Mbunge wa Mtwara Mhe. Hassan Seleman Mtenga alimwambia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kuwa pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na NHC ana wasiwasi kuwa Wizara ya Afya haijawa tayari kuhakikisha Hospitali hiyo inatoa huduma za tiba kama walivyomuahidi Makamu wa Rais.
Naye Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa Mkoa wa Mtwara Bi. Angeline Magazi akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, alimueleza Katibu wa Itikadi na Uenezi kuwa mradi huo utakaogharimu Shilingi Bilioni 15.8 hadi kukamilika umefikia asilimia 97 na kazi zinazoendelea zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba 2021, ambapo Shirika litakabidhi jengo hilo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo, Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndugu Shaka Hamdu Shaka na Katibu wa Vijana Taifa Ndugu Kenani Kihongozi wako katika ziara ya Mikoa ya Kusini mwa Tanzania ya Lindi Mtwara na Ruvuma ili kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 -2025.
Leo Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo yupo katika Wilaya ya Masasi na Katibu wa Vijana Taifa Ndugu Kenani Kihongozi yupo Wilayani Nanyumbu.