**************************
Na Joseph Lyimo, Simanjiro
WAVUVI wanaofanya shughuli zao kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kufika kwenye vituo husika na kupatiwa chanjo ya Covid-19 na kuachana na dhana potofu.
Wavuvi hao wa Bwawa la Nyumba ya Mungu wametakiwa kupata chanjo hiyo kwani hukutana na makundi ya wadau wa uvuvi wa samaki kutoka Wilaya tatu za Simanjiro na Mwanga na Moshi za Mkoa wa Kilimanjaro.
Mmoja kati ya wavuvi wa Kijiji cha Nyumba ya Mungu Kata ya Ngorika Joseph Okoth amesema baadhi ya watu wamekuwa wanazusha dhana potofu ili watu wasipatiwe chanjo.
Okoth amesema baadhi yao wapotoshaji hao hawana elimu ya ugonjwa wa Corona lakini wamekuwa mafundi wa kuzusha habari potofu ili hali hakuna faida wanayoipata.
“Wewe huna utaalamu wa afya wala hujui chochote juu ya virusi vya Corona lakini unatoa elimu potofu juu chanjo ya Covid-19 utapata faida gani?” amehoji Okoth.
Mvuvi mwingine Davis Mosses amesema alichanja kwenye zahanati ya Kijiji cha Nyumba ya Mungu hivyo anafanya shughuli zake bila hofu ya Corona.
Mosses amesema baada ya kuona na kusikia kwenye vyombo vya habari namna watu wanavyopata shida kwenye hospitali mbalimbali kwa kuvuta hewa kwa kutumia mitungi alifika na kuchanjwa Agosti 5 mwaka huu.
“Pamoja na mimi kuwa nimechanja bado navaa barakoa, natembea na kitakasa mikono na kila nikifika eneo jingine nanawa na maji tiririka ili nisipate maambukizi ya Covid-19 japokuwa nimeshapata chanjo,” amesema.
Mfanyabiashara wa samaki Mariam Hamis amesema wadau wa uvuvi wanapaswa kupata chanjo hiyo kwani wanakutana na makundi mbalimbali ya watu tofauti hivyo wanapaswa kujikinga.
Mariam amesema wavuvi hao hukutana na wasafiri wanaosafirisha samaki maeneo mbalimbali ya nchi hivyo chanjo ya Covid-19 itawasaidia kuliko kufanya shughuli zao bila kuchanja.
“Wataalamu wanasema ukichanja unaweza kupata Corona ila itakuja kwa heshima na utapona tofauti na mtu asiyechanja hivyo tuchangamkie fursa hii,” amesema.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Ngorika Albert Msole amewaasa wavuvi na wananchi wa eneo hilo kuchangamkia fursa ya kupata chanjo kwani inapatikana.
Msole amesema chanjo hiyo inapatikana kwenye zahanati iliyopo kwenye Kijiji cha Nyumba ya Mungu, hivyo wananchi wa eneo hilo wajitokeze kupata chanjo hiyo.
Amesema hivi karibuni zahanati ya kijiji hicho ilipatiwa kiasi cha dozi 100 ya chanjo hiyo ambapo hadi hivi sasa asilimia 70 ya chanjo hiyo imeshatumika kwa watu kujitokeza na kuchanja.
“Wananchi wa eneo hili hususani wavuvi waachane na habari potofu za kwenye mitandao kuwa chanjo hiyo ina matatizo hivyo, wafuate ushauri wa wataalamu kuwa chanjo haina madhara,” amesema Msole.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt Aristidy Raphael amesema chanjo ya Covid-19 iliyopokelewa kwenye Wilaya hiyo ni dozi 1,000.
Dkt Raphael amemaliza kwa kusema mwitikio wa watu kushiriki kwenye chanjo hiyo siyo mbaya kwani watu zaidi ya 800 wameshajitokeza kuchanja hadi hivi sasa.