TAMWA ZNZ
IMEBAINISHWA kuwa vyombo vya habari bado vinakabiliwa na ukosefu wa maudhui ya kutosha ya kiuandishi yatokanayo na uchambuzi wa masuala mbalimbali katika jamii jambo ambalo linapelekea matatizo na kero za wananchi kushindwa kutaftiwa ufumbuzi kwa wakati.
Hayo yamebainishwa kupitia utafiti maalum uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) ulioangazia ulinganisho kati ya wanasiasa wanawake na wanaume katika vyombo vya habari kwa kipindi cha novemba hadi desemba 2020.
Akiwasilisha taarifa ya utafiti huo kwa waandishi wa habari, mhadhiri wa chuo kikuu, Dkt. Abubakar Rajab alisema hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali ikiwemo mifumo ya sera za uendeshaji wa vyombo vya habari kutotoa fursa ya habari za namna hiyo.
Aidha alieleza kuwa sababu nyingine ni waandishi kukosa uthubutu wa kuandika habari za aina hiyo na badala yake kubakia kuandika habari za matukio.
Alisema, “bado waandishi wanakwenda kuandika walichotumwa kuandika na hawafanyi juhudi za kuandika uchambuzi ambapo hii inatokana na eidha waandishi ni woga sana katika kuchambua na kukosoa hivyo wanashindwa kuonesha madhaifu yaliyopo katika jamii.”
Akizungumzia kuhusu aina za habari zinazoandikwa zaidi katika vyombo vya habari alielezea kuwa vyombo vingi vinaandika na kutoa zaidi habari za kisiasa kuliko mada nyingine.
“Tumebaini kwamba kwa asilimia 95 waandishi wanaandika habari za kisiasa kuliko nyingine na habari hizi zaidi ni zile habari za matukio ya mikutano ya wanasiasa ambazo zinaelezea nani kasema nini pekee,” alisema Dkt. Abubakar.
Kuhusu ulinganisho kati ya wanasiasa wanawake na wanaume katika vyombo vya habari mhadhiri huyo alisema licha ya vyombo kuandika habari za wanawake lakini bado juhudi zaidi zinahitajika kwa waandishi kuongeza nguvu katika uandishi wenye kulenga kuchambua ushiriki wa wanawake katika nafasi hizo na kuzipa kipaumbele katika vyombo vyao.
Alitaja Gazeti la Zanzibar leo kuwa licha ya kuwa na idadi nyingi ya habari zinazohusu wanawake wanasiasa lakini habari hizo kwa kiwango kikubwa ziliwekwa katika kurasa za ndani ya gazeti hilo.
Alibainisha, “asilimia 94 ya makala zinazohusu wanawake wanasiasa katika gazeti la Zanzibar Leo, habari zote ziliwekwa katika kurasa za ndani ya gazeti kuliko kurasa za mbele. Hivyo bado kunahitajika nguvu ya ziada ya kuwashawishi wahariri kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume wanasiasa katika vyombo hivyo.”
Katika hatua nyingine utafiti huo umebainisha kuwa taarifa nyingi zinazotolewa katika vyombo vya habari waandishi wengi wanaoandika habari kuhusu wanawake wanasiasa ni wanaume kwa asilimia 83.
Kutokana na hali hiyo mhadhiri huyo alisema ipo haja kwa waandishi wa habari na vyombo vya habari kubadili mwelekeo wa uandishi na utoaji wa habari ili kusaidia utatuzi wa matatizo ya wananchi.
“Lazima muwe na uwezo wa kuandika aina zote za habari kama uchambuzi, Makala na maoni ili kuondokana na uandishi huu wa matukio,” alisema.
Aidha aliongeza, “mnatakiwa kuwa watetezi wa kulingania haki za wananchi ikiwemo kutetea ushirikishaji wanawake katika uongozi ili kuweza kufikia lengo la upatikanaji wa usawa wa kijinsia katika vyombo vya maamuzi.”
Utafiti huo wa ulinganisho kati ya wanasiasa wakike na wanaume katika vyombo vya habari ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ushirikishaji wanawake katika uongozi unaotekelezwa na TAMWA Zanzibar, PEGAO na ZAFELA kwa kufhadhiliwa na Ubalozi wa Norway chini.