*******************************
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT) Mkoa wa Njombe Scolastika Kevela amesema Rais Samia Suluhu Hassan anatosha kusimama katika nafasi ya kugombea nafasi ya Uraisi Mwaka 2025 na kusisitiza wao kama wanawake wa Mkoa wa Njombe wapo naye bega kwa bega katika hilo hadi ushindi.
Scolastika ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, ameyasema hayo ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan autangazie Umma kuwa lolote linawezekana katika kusimama kugombea hicho panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.
“Sisi kama wanawake wa Mkoa wa Njombe tunasema Rais Samia Suluhu mitano tena, usiku na mchana tutakuwa naye, yeye ndiy Rais wetu na atakuwa Rais wetu miaka mitano mingine kuanzia Mwaka 2025” alisema Scolastika Kevela
Awali akizungumza katika kongamano la Demokrasia lililofanyika katika ukumbi wa Karimjee na kuwahusisha wanawake ,jana Rais Suluhu Hassan alisema Mwaka 2025 Tanzania itamweka Rais mwanamke endapo watafanya vitu vyao vizuri na kushikamana.
“SASA ndugu zangu, Rais mwanamke tutamweka mwaka 2025. Ndugu zangu, mwaka 2025, tukifanya vitu vyetu vizuri, tukishikamana, tukimweka Rais wetu, tutakutana hapa kwa furaha kubwa sana”
“Wameanza kutuchokoza, kuandika kwenye vigazeti eti Samia hatasimama, nani kawaambia? Fadhila za Mungu zikija mikononi mwako usiziachie, hizi ni fadhila za Mungu ndugu zangu” alisema Rais Samia Suluhu Hassan katika kongamano hilo
“Wanawake wamefanya kazi kubwa ya kuleta uhuru wa nchi hii, wanawake tumefanya kazi kubwa kujenga siasa za nchi hii, tumebeba sana wanaume kwenye siasa za nchi hii, leo Mungu ametupa baraka mikononi, tukiiachia Mungu atatulaani.” aliongeza Rais Samia akizungumza na wanawake hao
Akizungumzia kauli hiyo Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe alisema Rais Samia kwa kipindi kifupi tangu ashike madaraka, Rais Samia Suluhu Hassan amelifanyia Taifa hili mambo makubwa na kuionyeshea dunia kipaji chake cha kuongeza.
Alisema kwa kipindi cha takribani miezi sita cha uongozi wake, amelifanyia taifa mambo makubwa huku akiendelea kuweka uwiano sawa wa wanawake na mwanamme katika uongozi jambo linalompa sifa kimataifa.
Alisema imani yake muda ulifika Rais Samia mbali na kuungwa mkono na wanawake na idadi kubwa ya wanawake pia ataungwa mkono na wanamme katika uchaguzi huo na hatimaye kumchagua kuliongeza Taifa hili kupitia kura za wananchi.
Alisema nafasi uliyonayo kwa sasa ni ya kikatiba ambayo tangu ameshika ameitumikia kikamilifu kama viongozi wengine waliopita jambo linaloonyesha kuwa ana kipaji cha uongozi.