Na.Alex Sonna,Dodoma
BARAZA la Taifa la Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), limeazimia kumsimamisha Rais wake Leah Ulaya kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba.
Akitangaza uamuzi huo kwa waandishi wa habari leo, Makamu wa Rais wa CWT, Dinna Mathamani amesema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao cha dharura cha baraza hilo kutokana na wanachama kutokuwa na imani naye ambapo waliandika hoja binafsi.
“Mwalimu mmoja amewasilisha hoja tisa na mwalimu mwingine kuwasilisha hoja nne ambazo jumla zilikuwa 13 ambazo zilijadiliwa na baada ya hoja zote kusomwa na Leah kutoa ufafanuzi, wajumbe hawakuridhika na majibu na hivyo kufikia maamuzi ya kumsimamisha kwa mujibu wa sharia,” amesema Dinna.
Amesema, baada ya kutoridhika na majibu, wajumbe wengi walitaka kiongozi huyo asimamishwe hadi mkutano mkuu utakapofanyika 2022 ndio utakaotoa maamuzi ya mwisho kwamba aendelee kuwepo madarakani ama kuondolewa wakabisa.
Amebainisha amesimamishwa kwa kupigiwa kura na waliotaka asimamishwe ambazo ni 131 kati ya kura 177 zilizopigwa.
Ametaja baadhi ya hoja zilizofanya na Leah kusimamishwa ni pamoja na kutengeneza mazingira ya kutofanyika uchaguzi wa kujaza nafasi ya katibu mkuu baada ya aliyekuwepo kufariki.
“Uchaguzi ulitakiwa ufanyike mwaka 2018 kwa ajili ya kujaza nafasi hiyo, kutokana na sintofahamu za hapa na pale, kulikuwa na mazingira yaliyosababisha uchaguzi huo usimamishwe na wajumbe wote walishafika eneo la tukio na hivyo kukitia chama hasara iliyosabishwa na uzembe wa Leah” amesema
Pia, ametaja sababu nyingine “kulikuwa na taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali, ambapo baada ya ukaguzi walipelekewa taarifa katika vikao vyao huku kurasa zilizomtaja na kumtaka Leah awajibike hazikuonekana, Wajumbe wa kamati ya utendaji hawakuziona hizo karatasi zilizomtaka awajibike kwa kushindwa kusimamia taasisi vizuri na hivyo kushindwa kutoa maamuzi kwa wakati.”