Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani akifungua kikao leo cha pande mbili za Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS) na Jumuiya ya Wanyamapori ya ISAWIMA cha kujadili utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu alilitoa hivi karibuni la kutaka magogo yaliyovunwa kiharamu yauzwe kwenye mnada.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa huduma za Mistu Tanzania(TFS) Mohamed Kilongo akielezea leo utaratibu uliofanyika wa kuhakiki idadi ya magogo ambayo yalivunwa kiharamu kwenye hifadhi ya ISAWIMA ambayo yataanza kuuzwa kwenye mnada utafanyika Jumatatu ijayo.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kanda ya Magharibi Ebratrino Mgiye akitoa ufafanuzi leo kuhusu zoezi la mnada wa Magogo ambayo yalivunwa kiharamu katika msitu wa Isawima.
Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima Hamis Katabanya atoa shukurani leo kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa juhudi zake za kuwakutanisha na TFS na hatimaye kufikia muafaka iliondoa mvutano uliokuwepo kuhusu gharama za ukusanyaji wa magogo yaliyovunwa kiharamu.
*******************************
NA TIGANYA VINCENT
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Buriani amewataka Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania(TFS) kuhakikisha inatekeleza makubaliano waliofikia na Jumuiya ya Msitu wa Hifadhi ya Isawima kulipa gharama walizotumia katika ukusanyaji wa mgogo yaliyovumwa kiharamu kwenye Msitu wa Hifadhi.
Alisema hatua hiyo itasaidia kwa kila upande kupata haki yake kulinga na majukumu iliyoyatekeleza kwenye zoezi zima la ukusanyaji magogo hayo na kuyapiga mnada.
Balozi Dkt. Batilda ametoa kauli hiyo leo wakati akiongoza kikao cha pande mbili cha kujadiliana utekelezaji wa agizo lilitolewa na Waziri Mkuu hivi karibuni akiwa ziara Mkoani Tabora katika eneo la Isiwama la kutaka magogo yaliyovunwa kwa njia haramu yapigwe Mnada.
Mkuu huyo wa Mkoa aliagiza TFS ishirikiane na ISAWIMA katika kukokotoa gharama halisi za ukusanyaji wa magogo kutoka yaliopatikana kwenye maeneo ya msitu kwa kuzingatia Jiografia na kuzingatia kipindi walichoyakusanya magogo hadi kuyafikisha katika Kijiji cha Wachawaseme na Mpwanga.
Alisema gharama ya shilingi 80,000/= kwa gogo moja inayodaiwa na Jumuiya ya ISAWIMA inaweza ikawa kubwa na kuongeza kuwa ni vema wakajiridhisha kabla ya kulipa kiasi hicho kwa gogo moja.
Aliongeza baada ya uhakiki kufanyika malipo ya gharama halisi za ukusanyaji yalipwe ndani ya muda mchache baada ya kumalizika mnada.
Aidha Balozi Dkt. Batilda ameitaka TFS kusaidia kuunga mkono juhudi za wananchi katika miradi ya maendeleo kwenye maeneo ambayo yalikuwa yanaunda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameomba TFS iwasaidie wafugaji wa nyuki mizinga 10,000 ya kisasa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali mkoani humo.
Alisema uongozi wa Mkoa unaendelea na utaratibu wa kufufua Chama Kikuu cha Wafugaji wa Nyuki kwa lengo la kuwasaidia ili waweze kuwa na mizinga ya kisasa ambayo itawaongezea kipato.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi kutoka TFS Mohamed Kilongo alisema taratibu za kuhakiki idadi ya magogo ambayo yalivunwa kiharamu ISAWIMA umekamilika na mnada utafanyika Jumatatu ijayo.
Kwa upande wa Katibu Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Isawima Hamis Katabanya amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa juhudi zake za kuwakutanisha na TFS na hatimaye wamefikia muafaka na kuondoa mvutano uliokuwepo.