Mwenyekiti wa The Desk & Chair Foundation akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hiyo ukiwemo wa madawati kabla ya kukabidhi madawati 348 ya kupunguza changamoto ya uhaba wa madawati wilayani Nyamagana jana.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akizungumza baada ya kupokea madawati 348 kwa aniaba ya walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo , Ilemela na Dodoma jana.
Yasin Hassan wa tatu kutoka kulia, akipokea madawati kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi (wa pili kushoto) kwa ajili ya kituo cha Madrasati Fisabillilah cha Ilemela.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi, kushoto akimkabidhi moja ya madawati Mkuu wa shule ya msingi Holy Face ya Dodoma, Sister Drosa Alphonce (mwenye kilemba cheupe jana.
Diwani wa Nyamagana Bhiku Kotecha akitoa shukurani kwa niaba ya Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine, kwenye hafla ya kupokea msaada wa madawati 348.Picha zote na Baltazar Mashaka
MKUU wa Wilaya ya Wilaya ya Nyamagana,Amina Makilagi, amesema wilaya hiyo ina uhaba wa madawati 17,000 kwa shule za msingi na sekondari.
Mkuu huyo wa Wilaya alizitaja baadhi ya shule zitakazonufaika kwa mgawo wa madawati hayo 238 ni Buhongwa 55,Mkolani 35,Nyamalango 30,Nyegezi 30, Mabatini 30,Igoma 30 na Kapripoint 25.
“Ingawa mna waenzi wazazi wenu, taasisi hii ni ya kitaifa na kimataifa inayofanya kazi kubwa ya kuisaidia serikali kuhudumia jamii, mnafanya haya bila kubagua lakini serikali haina cha kuwalipa na Mungu atawalipa,”alisema Mkilagi.
Meghjee alisema mahitaji ya madawati nchini ni milioni 1.3 ambapo Jiji la Mwanza ni 17,000, hivyo taasisi hiyo imechangia madawati 348 kati ya hayo 50 imepewa shule ya Holy Face ya Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma na kituo cha Madrasati Fisabillilah cha Ilemela, kikinufaika kwa madawati 25 na 238 yatasambazwa kwa baadhi ya shule za wilayani Nyamagana.
Alifafanua awali walishasambaza madawati zaidi ya 4000 kwenye shule za msingi na sekondari Kanda ya Ziwa na Zanzibar, wamekarabati mengine 1000,wamejenga madarasa 12 kati ya hayo mawili kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu na wamejenga matundu 311 ya vyoo bora kwenye taasisi za umma, dini na kijamii.
Aidha wamejenga jengo la CT Scan, matundu 38 ya vyoo,kuboresha mfuko wa maji,kujenga banda la kupumzikia na kununua vifaa tiba kwenye hospitali ya Sekou Toure, huduma ambazo zimekuwa na tija kwa jamii kwa kutoa ajira na watu kulipwa ujira wao kabla ya jasho lao kukauka.
“Pamoja na mafanikio ya tuliyopata, tunakabiliwa na changamoto ya maombi mengi kutoka idara zote na taasisi mbalimbali hasa upande wa wagonjwa na elimu,nyingine ni miradi ya midogo ya utoaji mikopo bila riba na ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu na wajasiriamali,lakini wamekataa kurejesha,”alisema Meghjee.
Meghjee alisema tangu waanze kuhudumia jamii kwenye sekta ya afya, maji na elimu wamefanikiwa kugusa maisha ya jamii wakilenga kuleta mafanikio katika maendeleo na ustawi wa jamii hivyo serikali isiste kuwaeleza mapungufu yao licha ya changamoto wanazokumbana nazo.