Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa pili kulia) akizindua Mpango Kabambe wa Mji wa Geita tarehe 15 Sept 2021 mkoani Geita. Aliyevaa miwani ni Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Constantine Kanyasu.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kulia) akimkabidhi Mpango Kabambe wa Mji wa Geita Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Constantine Kanyasu kwa niaba ya wananchi wake wakati wa hafla ya uzinduzi mpango huo tarehe 15 Sept 2021 mkoani Geita.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa uzinduzi Mpango Kabambe wa Mji wa Geita tarehe 15 Sept 2021 mkoani Geita.
******************************
Na Munir Shemweta, GEITA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezindua Mpango Kabambe wa Mji wa Geita 2017-2037 na kuitaka halmashauri ya mji huo kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa mpango huo bila kuruka hatu za utekelezaji.
Alisema, mkoa wa Geita umebahatika kuwa na shughuli nyingi zikiwemo za uchimbaji dhahabu na kuufanya mkoa huo kupewa jina la ‘mji wa dhahabu’ ambapo alisistiza kuwa fursa dhahabu ikitumika vizuri basi italeta mapinduzi ya haraka ya kiuchumi na kijamii kwenye mji huo.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Geita ina wachimbaji wengi wa madini na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaangalia namna bora ya kuwatambua wachimbaji wadogo wote ili waweze kupata fursa ya kumililkii maeneo yao kwa kuwa na hati ya umiliki wa ardhi..
‘’Wachimbaji wadogo wana leseni za uchimbaji madini lakini mgogoro huku juu ni mkubwa sana kwa sababu tu hawajatambulika ‘’ alisema Dkt Mabula.
Uzinduzi wa Mpango Kabambe wa Mji wa Geita 2017-2037 ulifanyika tarehe 15 Sept 2021 katika mji huo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani, wawakilishi wa taasisi za serikali, watumishi wa sekta ya ardhi, viongozi wa dini na wananchi wengine.
Aliongeza kwa kusema kuwa, hata namna ya kuwawezesha wachimbaji hao wadogo kupitia ardhi nako kutawawezesha kufanya kazi kwenye madini na huku pia wakipata mkopo benki kupitia hati za umiliki ardhi kutawawezesha kufanya kazi zao vizuri.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Mpango Kabambe uliozinduliwa katika utekelezaji wake utaenda sambamba na kuwawezesha wachimbaji wadogo aliowaeleza kuwa wako wengi kuwa na uhakika na salama za miliki zao katika maeneo wanayofanyia kazi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Constatine Kanyasu alisema, Mpango Kabambe uliozinduliwa unatoa dira ya mji huo kuelekea kwenye manispaa kwa kuwa haiwezekani kuwa na Manispaa isiyokuwa na mpango na kusisitiza kuwa yeye na wananchi wake wamefarijika sana kwa kuzinduliwa mpango huo kabambe wa Mji wa Geita.
Naye Mkurugenzi Msaidzi katika idara ya Maendeleo ya Makzi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Imaculate Senje aliiomba halmashauri ya Mji wa Geita kuhakikisha wakati wa utekelezaji wake inahifadhi maeneo yote yaliyoanishwa katika mpango kulingana na mahitaji na kutolea mfano kama eneo limetengwa kwa ajili ya viwanda basi lihifadhiwe kwa shughuli hiyo.
Halmashauri ya Mji wa Geita ilianzishwa na kutangazwa rasmi mwaka 2022 na ndiyo makao makuu ya mkoa wa Geita. Halmashauri hiyo ni kitovu cha shughuli nyingi za kiutawala , kijamii na kiuchumi kwa mkoa wa Geita na hali hiyo inasababisha ukuaji wa haraka wa idadi ya watu na shughuli za kiuchumi katika mji huo.