Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti akisikiliza malalamiko wa vikundi vya wazao taka waliondamana hadi ofisini kwake jana kufuatia madai ya kutolipwa posho za miezi mitatu na Manispaa ya Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (kushoto mwenye tai) akiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya (katikati) wakitatua mgogoro wa madai ya posho za wazoa taka kufuatia kutoelewana na uongozi wa Manispaa hiyo jana.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya ametakiwa katika kipindi cha mwezi mmoja ahakikishe analipa madeni ya wazoa taka yanayokadiriwa kufikia Shilingi Milioni kumi ili waendelee na kazi ya usafi wa mazingira ya mji.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti jana (15.09.2021) wakati alipokutana vikundi vya wananchi wanaojihusisha na uzoaji taka ambao waliandama hadi ofisini kwake kuomba serikali iingilie mgogoro uliokwamisha malipo kwa miezi mitatu.
Wananchi hao waliojiunga katika vikundi vya uzoaji taka ili kutunza mazingira walichukua uamuzi wa kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kufuatia kutoelewana na uongozi wa manispaa juu ya uahalali wa madai yao ambapo wengine mikataba yao imesitishwa kwa sasa.
“Mkurugenzi simamia malipo ya wananchi hawa na kwa kuanzia lipa deni lao la mwezi Juni ifikapo kesho, kisha endelea na uhakiki wa miezi mengine ili hatimaye wote walipwe stahili zao na kazi ya usafi wa mji iendelee kwa ufanisi” aliagiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Akizungumza kwenye kikao hicho cha usuluhishi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema ni kweli wananchi hao wanadai posho zao za miezi mitatu na kilichochelewesha ulipwaji ni kazi ya uhakiki kubaini viwango sahihi kwa mujibu wa mikataba.
Mtalitinya aliongeza kusema anapitia kwa karibu mikataba ya makubaliano na vikundi hivyo ili fedha itakayolipwa iendane na hali halisi ya makusanyo na faini zilikosanywa na vikundi hivyo toka kwenye mitaa.
“Nafanya mapitio ya hesabu sahihi za madai yao. Awali walikuwa wanadai miezi kumi na tayari tumelipa miezi saba bado miezi mitatu ambayo ni Juni, Julai na Agosti mwaka huu” alisema Mtalitinya.
Katika hatua nyingine mwakilishi wa wazoa taka hao Leopodia Malema toka Mtaa wa Chemka alisema kikundi chao kinadai zaidi ya Shilingi Milioni tatu kutokana na usimamizi wa dampo na ushuru wa usafi.
Mkazi huyo wa Sumbawanga alisema kazi ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwenye mitaa ya Sumbawanga wamekuwa wakifanya kuzoa taka na kupiga faini watu wanaokiuka kanuni za usafi ambapo vikundi vingi vinaundwa na akina mama.