**************************
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Saidi Jafo amesema baadhi ya kemikali mbadala zilizopendekezwa kuwa rafiki kwa Ozoni, zimegunduliwa kuwa zinachangia ongezeko la joto duniani na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.
Ameyasema hayo leo akitoa taarifa kwa waandishi wa habari katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya hifadhi ya tabaka la ozoni.
Aidha amesema ili kulinda tabaka la Ozoni, Serikali za mataifa mbalimbali zilikubaliana kuunda Mkataba wa Vienna (Vienna Convention) wa Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 1985. Mkataba huu unasisitiza ushirikiano katika utafiti, usimamizi na ubadilishanaji wa taarifa za hali ya Tabaka la Ozoni kutokana na kupungua kwa matumizi yake.
Amesema vile vile ilianzishwa Itifaki ya Montreal (Montreal Protocol) inayohusu udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni na Itifaki hii ilipitishwa tarehe 16 Septemba, 1987.
“Lengo kuu la Itifaki hii ni kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni kwa ratiba maalum ili kutoa nafasi kwa mabadiliko ya teknolojia na upatikanaji wa kemikali mbadala hasa kwa nchi zinazoendelea”. Amesema Waziri Jafo.
Pamoja na hayo amesema ni muhimu tuzingatie kwamba juhudi za kila mmoja wetu zinatakiwa ili kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za biashara.