**********************************
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT), Gaudentia Kabaka ambaye pia ni mlezi wa Mkoa wa Singida ameanza rasmi ziara katika Mkoa wa Singida ambapo katika ziara hiyo ameambatana na kamati ya siasa ya Mkoa wa Singida,Sekretarieti ya Mkoa.
Katika ziara hiyo,Kabaka amekagua miradi mbalimbali ya Chama na Ile ya serikali, kwwa upande wa Chama, Kabaka amekagua ujenzi wa nyumba za makatibu wa wilaya ambapo alifika na kujionea ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT wilaya ya Singida Mjini ambapo amewapongeza Sana uongozi wa UWT hiyo,kwa jinsi wanavyosimamia ujenzi huo.
Kabaka amechangia kiasi cha Sh Milioni Mbili ili kuwashika mkono katika hatua hiyo ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UWT.
Pia amewapongeza Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Singida pamoja jumuiya za WAZAZI NA UVCCM kwa hatua nzuri waliyoifikia katika ujenzi wa nyumba za watendaji(makatibu wa wilaya).
Katika ziara yake hiyo, Mwenyekiti Kabaka amefanya vikao kwenye Mashina ya CCM ambapo amekutana na wanachama wa CCM wa Mashina hayo na amefanya kikao na viongozi mbalimbali wa Chama na jumuiya zake zote katika ngazi ya kata na wilaya ya Mkalama ikiwemo kamati ya siasa ya wilaya ya Singida Mjini na Sekretarieti yake.
Kabaka pia amefanya ziara katika wilaya ya Mkalama ambapo ametembelea kikundi cha wajasiriamali wanawake kiitwacho Mwanzo Mgumu,kikundi hiki kimenufaika na mkopo usio na riba kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mkalama, kikundi hiki kinajihusisha na biashara ya kununua mazao aina ya mahindi na badae kuyauza pia wanakikundi wanakopeshana kulingana na mkopo huo waliopata.
Sanjari na hayo, Kabaka amemtembelea hospitali ya wilaya ya Mkalama na kujionea hali ya ujenzi inavyoendelea katika majengo mapya matatu,katika hospitali hii, Kabaka amemsisitiza Mhandisi wa wilaya kuhakikisha ujenzi wanausimamia kwa weredi lakini pia ukamilike kwa wakati ili wananchi wa Mkalama wasipate shida ya matibabu hususan akina mama na watoto.