******************************
Na Mwandishi wetu, Babati
MBUNGE wa viti maalum Mkoani Manyara, Yustina Rahhi amsema wakulima wadogo nchini hutegemewa kwa asilimia 100 kulisha Taifa, hivyo wanapaswa kupewa kipaumbele katika kuboresha kilimo chao ili kiwe na tija zaidi.
Mbunge Rahhi ameyasema hayo Mjini Babati kwenye maadhimisho ya miaka 15 ya mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji wa mkoa wa Manyara (MVIWAMA).
Rahhi amesema wakulima wadogo na wafugaji nchini wanapaswa kuthaminiwa kwani huchangia kwa asilimia 100 usalama wa chakula kwa Taifa zima.
Amesema wakulima wadogo na wafugaji nchini huchangia asilimia 29 ya pato la Taifa hivyo siyo wakubezwa bali washikwe mikono katika kuendeleza shughuli zao.
“Kilimo kinachozalishwa na wakulima wadogo nchini kupitia mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, maharage, mafuta ya mimea, maziwa, mayai na nyama huchangia malighafi ya viwanda kwa asilimia 65,” amesema Rahhi.
Hata hivyo, amewata wakulima hao kuchangamkia fursa ya kilimo cha mafuta ya mimea hususani zao la alizeti kwani hivi sasa dunia nzima kuna mahitaji makubwa ya mafuta ya mimea.
Amesema mkoa wa Manyara upo kwenye ukanda mzuri wa kulima zao la alizeti na serikali imejipanda kuhakikisha mbegu zinapatikana za kutosha kupitia wakala wa mbegu wa ASA.
“Nawapongeza wakulima wadogo kuwa wanachama wa mtandao wao kwa kufanikiwa mambo yao kwani mnaweza kufanya utaratibu wa bei ya pembejeo za kilimo kwa bei nzuri,” amesema Rahhi.