**********************
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambaye pia ni Mlezi wa Mkoa wa Singida, Gaudentia Kabaka ameendelea na ziara yake mkoani humo ambapo ametembelea ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Singida Vijijini ambapo amefurahishwa na maendeleo yake huku akisisitiza kukamilika kwa wakati.
Kabaka ambaye ziara yake ilianzia Wilaya ya Singida Mjini anafanya ziara Mkoani humo kukagua miradi mbalimbali ya serikali na ile ya Chama cha Mapinduzi.
Pia Kbaka ametembelea na kujionea ujenzi wa Hospitali mpya ya wilaya ya Ikungi ambayo ni kubwa na ya kisasa zaidi huku akisisitiza matumizi mazuri ya fedha kwenye miradi hiyo.
Katika mradi huo wa Hospitali amewasihi viongozi wa serikali wa wilaya hiyo kuhakikisha wanapopewa fedha za miradi wanazisimamia kwa uaminifu ili zitumike kama zilivyokuwa zimekusudiwa.
” Kwa kweli nimefurahishwa sana na maendeleo ya ujenzi ya Hospitali hizi mbili za Wilaya ya Singida Vijijini na Ikungi, ujenzi wa Hospitali hizi za kisasa unatoa picha ni jinsi gani Serikali yetu inatekeleza kwa vitendo ilani ya CCM katika kumaliza changamoto ya Afya, nimpongeze Rais Samia kwa utekelezaji huo.
Maelekezo yangu kwa viongozi wa Serikali na hata Chama kuhakikisha mnatoa macho kweli kweli ili fedha zinazoletwa na Serikali hapa kutekeleza miradi hii zisiliwe, kuweni wakali katika usimamizi wa miradi hii, ujenzi pia ukamilike katika muda uliopangwa,” Amesema Kabaka.
Katika ziara hiyo pia, Kabaka ametembelea kikundi Cha wajasiriamali wanawake wanaonufaika na mikopo isiyo na riba inayotolewa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Ametoa wito kwa kikundi hicho kinachojishughulisha na ufugaji wa kuku chotara,Bata na nguruwe kuendelea kuhamasisha Wanawake wengine ili kukimbilia fursa hiyo ya kupata mikopo ya Halmashauri na kufanya biashara zitakazoinua vipato vyao na uchumi wa Nchi.
Kabaka amefanya kikao cha ndani cha wanachama na viongozi katika tawi la Puma wilaya ya Ikungi,ambapo amewakumbusha wana-CCM kuhakikisha wanalipa ada za uanachama na wale ambao bado hawajasajiliwa kwa mfumo wa elektroniki wajitahidi wasajiliwe pia viongozi wa mashina na matawi wajitahidi kufanya vikao vya kikatiba ili kuendelea kuimarisha uhai wa CCM.