Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amefungua warsha kwa
maafisa wa Serikali wanaoshiriki zoezi la uwekaji gharama katika mpango mkakati
elekezi wa maendeleo wa kanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa SADC –
RISDP ( Regional Indicative Strategic
Development Plan 2020
– 2030).
Warsha
hiyo inayoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
ambaye pia ni mratibu wa masuala ya kikanda kitaifa imeanza leo tarehe 15 hadi
22 Septemba, 2021 mjini Morogoro. Pia
imehudhuriwa na maafisa kutoka wizara zinazosimamia sekta za vipaumbele zilizoainishwa
katika Mkataba wa SADC wa mwaka 1992.
Sekta
hizo ni pamoja na; Amani, Usalama na Utawala
Bora; Maendeleo ya Viwanda na Mtangamano wa Masoko; Maendeleo ya Miundombinu
katika kusaidia Mtangamano wa Kikanda; Maendeleo ya Jamii na Watu; Jinsia,
Vijana, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia nchi na Usimamizi wa hatari ya Maafa; na
Usimamizi wa kimkakati wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kanda.
“Nimeelezwa
kuwa Warsha hii inajumuisha sekta mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
hasa zile zinazohusika moja kwa moja na utekelezaji wa itifaki na sera
mbalimbali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika. Ni faraja kuona mpo
katika ari kubwa kwa ajili ya kuikamilisha kazi hii muhimu, hivyo mkaweke mbele maslahi ya Taifa wakati wa kupanga gharama kwenye maeneo husika.” Alisema Balozi Fatma
Lengo
kuu la mpango huu ni kuimarisha ushirikiano katika Kanda kwa ajili ya
kuharakisha juhudi za kupunguza umaskini na hatimaye kufikia malengo ya
maendeleo ya kiuchumi na yasiyo ya kiuchumi. Mpango huu mpya umekuja baada ya
ule wa awali wa mwaka 2015 – 2020 kumalizika muda wake. Kimsingi mpango huu
mpya umetokana na Dira ya SADC ya mwaka 2020 – 2030 (Vision 2050)
Kadhalika, Balozi Fatma alitumia fursa hiyo
kuwashukuru Shirika la
Ujerumani (GIZ) kwa kukubali kufadhili shughuli hii na akawaahidi kuwa Serikali
itaendelea kuwapa ushirikiano kwenye programu na miradi mbalimbali inayotekelezwa
nchini na kikanda.
Zoezi hili linafanyika kufuatia maelekezo ya
Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Mendeleo kusini mwa Africa (SADC) uliofanyika
mwezi Agosti 2021 Lilongwe, Malawi. Mkutano huo ulizitaka nchi wanachama
kukamilisha zoezi hilo na kuwasilisha maoni yao kwa Sekretarieti ya SADC kabla ya
tarehe 30 Septemba 2021.
Mshauri Elekezi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Dkt. Tumaini Katunzi akifuatilia hotuba ya ufunguzi. |
Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Joshua Mponera akielezea ratiba ya warsha kwa washiriki wakati wa ufunguzi. |
Washiriki wakifuatilia ufunguzi wa warsha hiyo. |
Washiriki wakifuatilia ufunguzi wa warsha. |
Washiriki wakifuatilia ufunguzi wa warsha. |