Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Save the Mother and the Children of Central Tanzania (SMCCT) la mkoani Singida limewakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili sheria ndogo ndogo zitakazosaidia kumlinda mama na mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kupitia mradi wa utetezi dhidi ya mila potofu uliofadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Society (FCS)
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jana wilayani Ikungi mkoani hapa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Evalyen Lyimo alisema mradi huo unatekelezwa kwenye kata sita na vijiji 18 katika wilaya hiyo.
Alitaja maeneo mengine yatakayo pitiwa na mradi huo kuwa ni katika shule za msingi 26 pamoja na vilabu vya wanafunzi 26 ambapo kwa shule za msingi wana vilabu 20 na Sekondari vilabu sita ambavyo vinafanyakazi ya kupinga ukatili wa kijinsia.
Alisema utekelezaji wa mradi huo umeanza mwezi huu wa Septemba na utafikia tamati mwezi machi mwakani.
Lyimo alisema jana ndio wameanza kazi rasmi kwa kuwakutanisha viongozi wa kamati ya Mtakuwwa ngazi ya wilaya, kata na vijiji ili kuweza kupitia sheria ndogo ndogo zilizoandaliwa zitakazo saidia kuthibiti vitendo hivyo.
Alisema katika kikao hicho wamewakutanisha madiwani, maafisa watendaji wa kata, watendaji wa vijiji akiwepo na Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Alisema baadhi ya shughuli zitakazofanyika kupitia mradi huo ni kuwajengea uwezo walimu na viongozi wa vilabu vya watoto ili waweze kujifunza kukuza stadi,maarifa na mitazamo chanya katika kusaidia wanafunzi kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia pamoja na kutengeneza mpango endelevu wa vilabu vya watoto mashuleni.
Alisema shughuli nyingine watakayoifanya ni kuandaa kikao cha kimkakati cha kujifunza na kamati za ulinzi wa wanawake na watoto kuanzia ngazi ya wilaya, kata na vijiji kwa ajili ya kuimarisha mpango kazi wa utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na utoaji wa rufaa katika vijiji na kata hizo kwa siku mbili na katika baadhi ya shule.
Alisema changamoto kubwa wanazokutana nazo katika shughuli hizo za utetezi ni jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya suala zima la kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia unapotokea hasa pale unapofanywa na ndugu hivyo kesi hizo huishia nyumbani na kushindwa kupatikana kwa haki kwa muathirika na kukwamisha harakati za kutokomeza vitendo hivyo.
Aidha Lyimo alisema uchumi mdogo kwa waathiriwa wa vitendo hivyo huchangia kushindwa kutoa taarifa na akataja changamoto nyingine ni ugonjwa wa corona ambao umechangia kutofanya kazi hiyo kwa wakati kama walivyokuwa wamepanga.
“Mradi huu wa utetezi dhidi ya mila potofu ikiwemo ukeketaji na ukatili wa kijinsia,unalenga kuwafikia wanawake na wasichana wapatao 7,200 katika wilaya ya Ikungi ambapo hali ya unyanyasaji wa kijinsia sio nzuri sana”,alisema Lyimo.
Lyimo, ametaja baadhi ya malengo ya mradi huo kuwa ni kuongeza uelewa na kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukeketaji na kuimarisha mfumo wa utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia katika jamii hadi ifikapo machi mwakani.
Alisema mradi huo unatekelezwa katika kata sita za Ihanja, Iglansoni, Iseke, Minyughe, Muhintiri na Ikungi.
Mwezeshaji wa mradi huo, Japhet Kalegeya alisema Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) limetoa Sh.30 milioni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo kuanzia mwezi huu wa Septemba hadi mwezi Machi mwakani.
Alisema katika kutekeleza mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukati huo dhidi ya wanawake na watoto Mtakuwwa umelenga maeneo nane kuimarisha uchumi wa kaya, mila na desturi,mazingira salama, malezi,.kuimarisha mahusiano na kuziwezesha familia, utoaji wa huduma kwa waathirika wa ukatili pamoja na mazingira salama na stadi za maisha shuleni , uratibu na ufuatiliaji na tathmini.
Alisema shirika hilo katika maeneo hayo limejikita zaidi katika kuimarisha uchumi wa kaya, mazingira salama mashuleni na stadi za maisha ikiwa ni pamoja na usimamizi wa sheria.
Afisa Maendeleo ya Jamii Peter Mussa alisema sheria za kupinga vitendo hivyo zipo kwani zilikwisha tungwa na kuweza kukithi mazingira yaliyopo sasa lakini changamoto kubwa iliyopo dhidi ya ukatili wa watoto na wanawake ni namna ya usimamizi wa sheria hizo kwenye ngazi mbalimbali kwa maana watendaji wa vijiji, kata na wadau wengine ambao wanapaswa kufanya mikakati ambayo itawezesha sheria hizo ziweze kufanya kazi yake.
Alisema hakuna sababu ya kutunga sheria mpya wakati hizi zilizopo hazijafanyiwa kazi ipasavyo hivyo ni wajibu wa wataalamu na watendaji kuhakikisha kwamba wanasimamia sheria hizo na kikubwa zaidi wananchi waelimishwe ili kuzijua zikiwemo zinazohusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ombeni Komba alisema sheria hizo ndogo ndogo za vijiji kabla ya kutungwa kuna utaratibu wake ambao unatakiwa kufuatwa ili zisije kukinzana na sheria mama za nchi.
Alisema adhabu zitakazo tolewa kutokana na sheria hizo ni kiasi cha fedha kisicho zidi Sh.50,000 na kwa mtuhumiwa sio lazima kulipishwa faini ya fedha bali anaweza kupewa adhabu ya kufanya shughuli za maendeleo kama kuchimba shimo la choo, kuchota maji, kufyatua matofali na kadhalika.