*****************************************
Na Mwandishi wetu, Manyara
MTANDAO wa vikundi vya wakulima na wafugaji wa Mkoa wa Manyara (MVIWAMA) wameadhimisha miaka 15 ya kuwaunganisha kwa ufanisi.
Kaimu Mratibu wa MVIWAMA Donald Laizer akizungumza Mjini Babati jana kwenye maadhimisho ya miaka 15 ya mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji wa mkoa wa Manyara (MVIWAMA) amesema mtandao huo ulizinduliwa September 13 mwaka 2006.
Laizer amesema miongoni mwa mafanikio ya miaka 15 ni kuwaunganisha wafugaji na wakulima wadogo kuunda chombo chao cha utetezi.
Laizer amesema pia wakulima kutambulika na kushirikishwa kwenye ngazi za maamuzi, ujenzi wa miundombinu wezeshi na kuboresha masoko.
Amesema miaka 15 ya uwepo wa Mviwama ni fursa adhimu ya kujivunia kwa wakulima na wafugaji Manyara kuwa na chombo cha kuwaunganisha kutetea maslahi yao.
“Mviwama inaadhimisha miaka 15 ikijivunia na kutazama mbele inayojifunza ili kuzidi kuboresha huduma yake na kufikia lengo la kuboresha maisha ya wakulima na wafugaji wadogo,” amesema Laizer.
Amesema miongoni mwa maazimio yaliyofanywa na wakulima hao baada ya mchakato wa uanzishwaji wakati huo wakitambukika kama MVIWATA Manyara wakishirikiana na asasi ya FIDE, Mtandao wa vikundi vya wakulima na wafugaji wa Wilaya ya Monduli (MVIWAMO) na kuwezeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Ubelgiji la Trias.
“Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Anatoly Tarimo alisimika uongozi wa Kamati ya mpito iliyofanya kazi kwa miaka miwili chini ya ushauri elekezi wa Cornel Mushi na marehemu Magreth Nyanzari ikipata uzoefu kutoka MVIWAMO,” amesema.
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Manyara, Venance Msafiri amesema wakulima wanapaswa kuchangamkia fursa ya kilimo cha umwagiliaji.
“Kwenye mkoa wa Manyara kuna ekari 35,000 za umwagiliaji ila zinazotumika hazifiki hata ekari 10,000 hivyo wakulima waongeze juhudi kwenye kilimo cha umwagiliaji,” amesema Msafiri.
Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Yustina Rahhi amewapongeza MVIWAMA kwa kufanikisha maendeleo ya wakulima wadogo kwenye eneo hilo.
“Nilikuwa Mkuu wa idara ya kilimo kwenye Wilaya ya Mbulu na nimeshirikiana na MVIWAMA katika kuwajengea uwezo wakulima wetu kwa kipindi chote,” amesema Rahhi.
Mkulima mdogo wa kijiji cha Lemkuna, Kata ya Ngorika wilayani Simanjiro, Sara Daudi ameiomba serikali kufanikisha upatikanaji wa pembejeo kwa urahisi.
Mkulima wa alizeti wa wilaya ya Kiteto, Hamza Mngia amesema wadau wa mbegu za alizeti wanapaswa kuwahisha pembejeo ikiwemo mbegu hizo kwa wakati.