*************************
Na MWAMVUA MWINYI, CHALINZE
RAIS mstaafu wa awamu ya nne ,Jakaya Kikwete ameeleza nchi inakwenda vizuri ikiwemo kutatua changamoto za sekta mbalimbali ikiwemo afya ambapo imeendelea kutambua umuhimu wa kuongeza wigo wa huduma za dharula .
Aidha amesema, Rais Samia Suluhu Hassan analeta matumaini kwa watanzania kwa manufaa ya nchi ya leo na kesho .
Kikwete aliyasema hayo wakati wa kutembelea eneo litakalojengwa Mradi wa jengo la matibabu ya dharula katika hospital ya wilaya ya Chalinze iliyopo Msoga,uliofadhiliwa na kampuni ya ABBOTT fund ya nchini Marekani,kwa gharama ya bilioni 1.2.
Alisema, ABBOTT ,wameanza kusaidia na kushirikiana na serikali ya Tanzania, tangu Mwaka 2002 ambapo walianza na HIV,masuala ya ujenzi wa maabara na sasa miradi ya majengo ya dharula.
Alifafanua ,msaada uliotolewa kwa ajili ya jengo hilo ni bilioni 1.2 ikiwa ni sawa na dola 500,004(laki tano na nne) na tayari walishashiriki kusaidia masuala mbalimbali nchini ikiwemo kutoa vipimia VVU vipatavyo million moja.
“Sijafanikisha peke yangu hili ,mie niliweka msukumo ,lakini namshukur sana Naibu katibu mkuu wa Wizara ya afya ,wakati huo Dorothy Gwajima ambae ndie alipush suala hili ,Niseme tuu namshukur sana”alieleza Kikwete.
Kikwete aliiomba serikali ,itoe mafunzo kwa madaktari na watumishi wa afya kuhusiana na masuala ya dharula ili miradi kama hiyo itakapokamilika kusiwepo na changamoto ya ukosefu wa wataalamu wa dharula.
Hata hivyo,aliomba jamii na watumishi wa umma waendelee kumuunga mkono Rais Samia ,kwa kuchapa kazi na kuwataka vijana kujituma ili kujiepusha na kuwa mzigo katika jamii.
Nae Naibu waziri wa afya , maendeleo ya jamii ,jinsia ,wazee na watoto ,Godwin Morell ameeleza serikali imetenga kiasi cha sh.bilioni 187 kwa ajili ya kujenga kiwanda Cha chanjo za UVIKO19, zitakazozalishwa hapa nchini.
Aidha serikali imetenga bilioni moja kwa ajili ya kununua magari ya wagonjwa 150 ambayo yatasambazwa nchini ambapo kati ya hayo Jimbo la Chalinze litapatiwa gari moja kati ya hayo.
Morell alielezea, mbunge wa Jimbo la Chalinze ,Ridhiwani Kikwete aliomba milioni 418 na serikali imeridhia kutoa fedha hizo kwa awamu kwa ajili ya umaliziaji wa majengo ya ujenzi wa hospital ya wilaya.
Nae mbunge wa Chalinze, Ridhiwan Kikwete alisema juhudi zinaendelea kumaliza baadhi ya majengo katika hospital ya wilaya Chalinze, ambayo imetolewa bilioni moja katika ujenzi wa majengo matano ambayo yamefikia asilimia 83.
“Jengo linalokwenda kujengwa ni jengo tosha linalokwenda kuleta matokeo ya huduma bora za kiafya “
“Ilifika kipindi tulikuwa tumekata tamaa, ila nichukue nafasi hii kumshukuru Rais Samia Suluhu tumeweza kufanikiwa msamaha huo wa kodi “alisema Ridhiwani.
Mwakilishi kutoka ABBOTT ,Frenk Kanza alisema , kampuni hiyo inajishughulisha kutengeneza bidhaa za maabara dunia ila kwa msaada huu umetokana na fedha kutoka mfuko wa uwezeshaji wa masuala ya afya.
Aliishukuru Serikali kwa ,msamaha wa Kodi dollar 40,000 ,suala ambalo lilichangia kuchelewesha Mradi na kukwama kwa muda wa miezi miwili.
Alieleza, mradi huu utaleta Mapinduzi makubwa ya masuala ya kiafya katika wilaya ya Chalinze na mkoa wa Pwani.
Alibainisha,Wanatarajia kufanya kazi kwa kipindi Cha Mwaka mmoja ambapo wanatarajia September mwakani Mradi utakamilika na kuleta tija kwa jamii, na huduma hii itakuwa ya Kwanza kutolewa kwa ngazi ya wilaya kwa hapa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainab Abdallah alieleza, halmashauri imepata mradi mkubwa wa ujenzi wa EMD (jengo la dharula )toka ufadhili wa ABBOTT.
“Mradi huu unaokwenda jengwa kwenye hospital ya wilaya ya Msoga ,Ni matokeo makubwa ya maombi toka kwa Rais mstaafu awamu ya nne ,mzee Mrisho Jakaya Kikwete kwenda kwa Rais wa ABBOT (Marekani)
Zainab alisema ,mchakato wa Mradi umechukua zaidi ya Mwaka mmoja na kumshukuru kwa juhudi zake pia mbunge wa Chalinze Ridhiwan Kikwete kuusimamia Mradi wakati wote wa mchakato na ufuatiliaji wa kupatikana kwa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani .
Kwa upande wake ,mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amepiga debe kuwa mkoa una maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji hivyo itapendeza kiwanda Cha chanjo ya Uviko 19 ikajengwa mkoani Pwani.
Alieleza, pia mkoa umeshapokea bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa vituo vinne vya afya vinne vitakavyojengwa kwenye tarafa ,fedha ambayo imetokana na mihamala ya simu .
Kunenge alisema ,watasimamia Mradi huu kwani unakwenda kutatua changamoto za kiafya na wanashukuru inakwenda kufungua mkoa wa Pwani kimaendeleo.