*******************************
Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania imefanya kikao chake cha 216 tarehe 13 Septemba 2021 na kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha, pamoja na kupitia mwenendo mzima wa uchumi wa ndani na wa dunia.
Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha kwa kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2021 ambao uliwezesha uwepo wa ukwasi wa kutosha katika sekta ya benki, hali iliyojidhihirisha katika viwango vya riba katika masoko ya fedha ambavyo vimeendelea kubaki kati ya asilimia 3-5. Aidha, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 4.1 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai 2021 kutoka asilimia 3.6 kwa mwezi uliotangulia.
Kamati imebaini kuwa ukuaji wa uchumi wa dunia unaendelea kuimarika kutokana na janga la UVIKO-19, japo kwa kasi ndogo, na unatarajiwa kuendelea kuimarika siku za usoni. Mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa robo ya kwanza ya mwaka 2021, ulikuwa wa kuridhisha.
Uchumi wa Tanzania Bara, ulikua kwa asilimia 4.9, ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, uchukuzi, kilimo, uzalishaji viwandani, pamoja na uchimbaji wa madini.
Uchumi wa Zanzibar umekua kwa asilimia 2.2, ukilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.5 katika robo ya kwanza ya mwaka 2020. Ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuendelea kuimarika kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kutokana na uwekezaji unaoendelea katika miradi mbalimbali ya Serikali na kuimarika kwa uchumi wa dunia. Hali hii itachochea uwekezaji katika sekta binafsi na biashara.
Kasi ya mfumuko wa bei imeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3-5, sawa na malengo ya kitaifa na vigezo vya mtangamano wa kikanda. Mfumuko wa bei unategemewa kubaki ndani ya wigo huo.
Sekta ya nje imeendelea kukabiliwa na changamoto zitokanazo na UVIKO-19, hususani katika sekta ya utalii.
Aidha, mauzo ya dhahabu yaliongezeka kufikia dola za Marekani bilioni 3 kwa mwaka ulioishia Julai 2021. Akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubakia katika viwango vya kuridhisha na kufikia dola za Marekani bilioni 5.5, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa zaidi ya miezi 6, sawa na lengo la nchi na makubaliano ya jumuiya za kikanda.
Ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi ulikua kwa asilimia 11 kwa mwaka ulioishia Julai 2021, ukiwa ndani ya lengo la ukuaji wa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka 2021/22. Mikopo kwa sekta binafsi imeendelea kuongezeka, japo kwa kasi ndogo ya asilimia 4.1.
Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuimarika zaidi kutokana na hatua za ziada za kisera zilizochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania mwezi Julai 2021, pamoja na utekelezaji endelevu wa hatua za kuboresha mazingira ya biashara, na kuimarika kwa biashara za kimataifa na uwekezaji.
Kwa kuzingatia tathmini ya mwenendo wa uchumi wa hivi karibuni na matarajio ya kuimarika zaidi kwa uchumi wa ndani na wa dunia, Kamati ya Sera ya Fedha imekubaliana na pendekezo la Benki Kuu ya Tanzania la kuendelea kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuongeza ukwasi katika kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba 2021 ili kuongeza kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.