*******************************
Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
Mashua ijulikanayo kama ‘MV Adui Jamaa (Mbagara)’ imepata ajali na kuzama katika eneo la Simani (Songosongo) huko Mafia juzi,na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine wawili bado hawajapatikana kuokolewa.
Mashua hiyo ilikuwa na mzigo wa mwani ikiusafirisha kutoka kisiwa cha Jibondo wilayani Mafia kuelekea Kilwa.
Jumla ya watu sita walikuwa katika mashua hiyo ambapo wanne kati yao walikuwa ni wafanyakazi na wawili ni abiria.
Mkuu wa wilaya ya Mafia Eng. Martin Ntemo alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo mara baada ya kupokea taarifa hizo za kusikitisha aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo kwa kushirikiana na wadau wengine, kwenda katika eneo ilipotokea ajali ili taratibu za uokoaji zichukuliwe mara moja.
Aidha abiria mmoja aliyetambulika kwa jina Saidi Twalibu aliokolewa akiwa hai,ambapo Wataalam kutoka Hifadhi ya Bahari Mafia (HIBAMA) waliongoza zoezi la uokoaji.
Msako huo umedumu kwa siku tatu mfululizo tangu ajali itokee hadi maiti tatu zilipopatikana maeneo ya Rufiji na Kilwa.
Miili iliyopatikana imetambuliwa kuwa ni Amri saidi Amri (Ngenje) aliyekuwa nahodha wa chombo kilichopata ajali na Sadiki Abdallah Apondo ambao wote wamepatikana na kuzikwa katika kijiji cha Pombwe wilayani Rufiji.
Mwili mwingine ni wa Selemani Faki Hassani (Mnyaku) ambaye anazikwa katika kijiji cha Somanga wilayani Kilwa.
Jitihada zinaendelea za kuwatafuta wahanga wengine wawili ambao ni Hamza Shahame na Ahmadi Mwinyimanga, hatma yao bado haijajulikana.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia,Ntemo alielezea kusikitishwa kwake kwa kutokea ajali hiyo na anaungana na ndugu na jamaa wote waliopoteza wapendwa wao.
Ntemo amewasihi wamiliki na maendesha vyombo vya usafiri majini kuhakikisha wanazingatia masuala ya usalama hasa kwa kutozidisha uzito, kukagua mara kwa mara ubora wa vyombo vyao na kufuata miongozi mbali mbali inayotolewa na wataalam ikiwa nipamoja na hali ya hewa.