Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe akimsikiliza Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia baada ya taasisi hiyo kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 67 milioni kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto njiti katika hospitali ya Mkomaindo iliyopo halmashauri ya Mji wa Masasi mkoani Mtwara.
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia (wa pili kulia) akimkabidhi Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe baadhi ya vifaa Tiba vilivyotolewa na taasisi hiyo kwa hospitali ya Mkomaindo iliyopo katika halmashauri ya Mji wa Masasi ili kusaidia matibabu ya watoto njiti. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi Claudia Kitta na kushoto ni Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Masasi Dkt Amina Mushi.
Waziri wa Uwekezaji Geoffrey Mwambe (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Masasi Claudia Kitta (kushoto) wakipokea baadhi ya vifaa Tiba vilivyotolewa na kampuni ya Vodacom Tanzania Plc kupitia taasisi ya Vodacom Tanzanua Foundation kwa hospitali ya Mkomaindo iliyopo katika halmashauri ya Mji wa Masasi ili kusaidia matibabu ya Watoto njiti.
********************
Hospitali ya Mkomaindo ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara sasa itaondokana au kupunguza vifo vya watoto wachanga vitokanavyo na changamoto mbalimbali baada ya kukabidhiwa msaada wa vifaa tiba kutoka taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation.
Pia, watoto njiti katika hospitali hiyo wataondokana na changamoto ya kukaa wawili katika mashine maalumu (incubator) baada ya kusaidiwa nyingine na taasisi hiyo.
Wakikabidhiwa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh 67 milioni jana, Kaimu Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Masasi, Amina Moshi alisema vifaa tiba hivyo vimelenga kitengo cha uzazi kwa mama na watoto wachanga na hivyo vitasaidia kuboresha huduma za afya.
“Tulikuwa na changamoto ya vifaa tiba vinavyoweza kusaidia watoto wachanga kupata joto baada ya kuzaliwa na incubator kwa ajili ya watoto njiti waliozaliwa kabla ya kutimiza miezi tisa, vifaa vingine kama mashine za oksijeni vitawasaidia katika kupumua kwa wale wenye tatizo la kupumua baada ya kuzaliwa,”alisema Dkt Amina.
Alibainisha halmashauri hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya vifo vya watoto wachanga ambapo Januari hadi Disemba 2020 kulikuwa na vifo vya watoto wachanga 165 na Januari hadi Julai 2021 kumekuwa na vifo 63.
Alisema kwa upande wa vifo vya kina mama Januari hadi Disemba 2020 vifo vitokanavyo na uzazi vilikuwa 10 na Januari hadi Julai 2021 vilikuwa vifo sita hivyo msaada huo wa vifaa tiba vitasaidia sana kupunguza vifo hivyo.
“Pia tumepokea kitanda maalumu kwa ajili ya kumsaidia mama wakati wa kujifungua pamoja na vifaa maalumu vitakavyomsaidia mama pale atakapopata uchungu pingamizi kama vifaa vidogo vya uchunguzi, upatikanaji wa vifaa hivi tunaamini kwamba tatizo tulilokuwa nalo la vifo vya mama na watoto vitapungua kwa asilimia kubwa,”alisema Dkt Amina
Akizungumza Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Rosalynn Mworia alisema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na serikali katika maeneo mbalimbali kama afya na kilimo ili kugusa jamii hususani katika afya ya uzazi.
Alisema wamekuwa wakifanya uhamasishaji na kampeni mbalimbali kwa kutumia mtandao wa simu kwa kutuma ujumbe mfupi pamoja na njia nyingine za mawasiliano ili kupeleka taarifa mbalimbali za afya kama tatizo la fistula.
Alisema kukosekana kwa vifaa tiba kumekuwa kukisababisha majanga kwa kina mama na watoto kama wanaozaliwa wakiwa hawajatimiza miezi tisa.
“Vifaa hivi vitamsaidia mtoto kupata huduma ambazo hazijajengeka, vitamuwezesha kuishi, na tuna mifano ya watoto waliozaliwa njiti na sasa ni viongozi wanafanya kazi katika jamii,”alisema Rosalynn
Akizungumza Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geofrey Mwambe alizitaka taasisi za umma na wizara kuona zina wajibu wa kusaidia na kuhakikisha wawekezaji kwenye maeneo yao wanatekeleza sera ya kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility).
Alisema kwa kufanya hivyo watatengeneza ajira kwa vijana wengi kutokana na ukosefu wa ajira.
“Ukizifanikisha hizi taasisi au kampuni zikafanya biashara vizuri maana yake watapata faida kubwa zaidi hata asilimia 30 zinazokwenda serikalini itakuwa kubwa zaidi na hata ile asilimia kadhaa wanayotenga kupeleka kwa jamii itakuwa kubwa zaidi,”alisema Mwambe