*****************************
Na Joseph Lyimo, Simanjiro
Maji ni muhimu kwa viumbe vyote duniani, bila maji hakuna uhai, maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Maeneo mengi ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, ni nyanda kame hivyo sehemu nyingi kuna uhaba wa maji hivyo kusababisha wananchi kutembea umbali mrefu ili kufuata huduma hiyo.
Wanawake na watoto hutembea umbali mrefu wakiwa na wanyamakazi punda kwa ajili ya kufuata huduma ya maji kwenye maeneo mbalimbali.
Baadhi yao hutembea umbali wa kilomita 20 kutoka Kata ya Langai hadi Orkesumet au Kata ya Edonyongijape kufuata huduma hiyo hivyo kutembea kilomita 40 kuchota maji wakitumia punda.
Mkazi wa Kata ya Edonyongijape Esupati Paulo anasema wamezoea kufuata maji hadi Okresumet kwa kutumia punda hivyo kusababisha kushindwa kufanya shughuli nyingine za maendeleo kwa sababu ya kutembea umbali mrefu.
Esupati anasema kutokana na hali hiyo maji ni kipaumbele kwenye kunywa, kunywesha mifugo na matumizi mengine ikiwemo kupikia chakula ila siyo kwenye kuoga.
“Wanafunzi pia huchelewa kwenda shule kutokana na wao kusaidiana na wazazi wao kwenda kufuata maji asubuhi na kurudi nyumbani kasha ndiyo wanaelekea shuleni wakiwa wamechelewa,” amesema Esupati.
Amesema kutokana na hali hiyo uchumi wa baadhi ya wanawake pia hushuka kutokana na kutumia muda mwingi kufuata huduma ya maji badala ya kujishughulisha na kazi mbalimbali ikiwemo ujasiriamali.
“Tungeweza kufanya shughuli nyingine za kujiingizia kipato ila inabidi kwanza nifuate maji umbali mrefu kwani mimi ni mjasiriamali huwa nauza maziwa, ugoro na kushona shanga,” amesema.
Mkazi mwingine wa eneo hilo Nai Kishumu amesema kipaumbele cha jamii ya kifugaji ni mifugo hivyo vijana wao hutembea umbali mrefu kufuata maji ili kunywesha mifugo yao.
“Tunaiomba serikali ikamilishe mradi wa maji kwani itatusaidia Kwa namna moja au nyingine katika kutatua changamoto hii ya ukosefu wa maji,” amesema.
Mwanafunzi wa shule ya msingi Langai, Mosses Mollel amesema kutokana na kufuata huduma ya maji umbali mrefu huwa anachelewa kufika shuleni kwa muda muafaka kwani huwa inampasa akachote maji na punda kila asubuhi ndipo awahi shuleni.
“Kufuata huduma ya maji kilomita 20 kila siku siyo jambo dogo kwani shuleni hufika saa tano asubuhi hivyo nakosa masomo kwa vipindi vinne ambapo wenzangu huwa wanakuwa wamesoma,” amesema.
Mwanafunzi huyo ni miongoni mwa wanafunzi wanaokosa ipasavyo haki yao ya msingi ya kusoma na kujumuika na wenzake.
Majukumu ya Wakala wa Maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA yametajwa na kufafanuliwa katika kifungu cha 43 cha Sheria ya Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya mwaka 2019.
Kwa ujumla, RUWASA ina wajibu wa kuendeleza miundombinu kwa kufanya ujenzi na usimamizi wa ujenzi wa miradi ya maji na pia kusimamia utoaji wa huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira vijijini.
Katika kutekeleza jukumu hilo, RUWASA inafanya shughuli zifuatazo ikiwemo kuandaa mipango, kusanifu miradi ya maji, kujenga na kusimamia uendeshaji wake.
Kuendeleza vyanzo vya maji kwakufanya utafiti wa maji chini ya ardhi nakuchimba visima pamoja na kujenga mabwawa.
Kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu ya maji vijijini.
Kutafuta fedha kwa ajili ya uendeshaji ili kuwezesha RUWASA kutekeleza majukumu yake na kushirikiana na wadau mbalimbali katika masuala yanayohusu utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira vijijini.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Simanjiro mhandisi Joanes Martin anasema upatikanaji wa maji kwenye eneo hilo ni asilimia 56.1.
Mhandisi anasema lengo lao ni kuhakikisha maji yanapatikana kwa wananchi wote kwenye Wilaya ya Simanjiro kwa asilimia 85 kama ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inavyotaka.
Amesema kwa mwaka jana 2020 na mwaka huu 2021 visima tisa vilichimbwa kwenye Wilaya ya Simanjiro ila baadhi ya wananchi wa eneo hilo walijaza mawe visima vitano.
“Baadhi ya wananchi walijaza mawe kwenye visima tulivyochimba kwenye kata za Shambarai, Kimotorok, Terrat, Kijiji cha Sukuro Kata ya Komolo na Kijiji cha Kambi ya Chokaa Kata ya Naisinyai,” amesema mhandisi Martin.
Hata hivyo, amesema walifanikisha kukamilisha uchimbaji wa visima hivyo kwa kutumia gharama nyingine na hivi sasa maji yanapatikana kwenye maeneo hayo yaliyojazwa mawe kwenye visima.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, hivi karibuni alifanya ziara kwenye Wilaya ya Simanjiro na kuwapongeza RUWASA kwa namna wanavyofanya kazi yao ya kuhakikisha wananchi wanapatiwa maji.
“Maeneo mengine mmefanya kazi ya kuchimba visima na fedha kubaki na mkatumia fedha hizo kukamilisha miradi mingine hongereni sana RUWASA kwa kufanya hivyo,” amesema Makongoro.
Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, RAS Caroline Mthapula amewataka wananchi wanaoharibu miundombinu ya maji kwa kuweka mawe kwenye visima waache mara moja.
“Serikali inatumia fedha nyingi katika kuhakikisha inafanikisha wananchi kupatiwa maji lakini wengine wanakwamisha kwa kutumbukiza mawe kwenye visima jambo ambalo linasababisha kuongezeka kwa gharama za kuchimba visima,” amesema Mthapula.