Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga (kulia), akifafanua jambo kwa wataalam wa Wakala huo, TANESCO na Mkandarasi wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida, Septemba 9, 2021. Wa pili – kulia ni Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Julius Kalolo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (katikati) akizungumza na Mkazi wa Kitongoji cha Mlewa wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida, Elipendo Warioba wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Septemba 9, 2021.
Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini ukiwa katika ziara kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida, Septemba 9, 2021.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (kushoto) akisisitiza jambo kwa Wataalam wa REA, TANESCO na Mkandarasi wakati wa ziara ya Bodi wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida, Septemba 9, 2021. Wa pili – kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Msimamizi wa Miradi ya Umeme Vijijini, Kanda ya Magharibi, Mhandisi Oscar Migani (wa tatu-kulia), akifafanua jambo kwa Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo mkoani Singida, Septemba 9, 2021.
**************************************
Veronica Simba – Singida
Bodi ya Nishati Vijijini imewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuishirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi hiyo ili iwe yenye tija.
Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Julius Kalolo alitoa msisitizo huo Septemba 9 mwaka huu, wakati wa ziara ya Bodi mkoani Singida kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Akifafanua, alieleza kuwa wananchi na viongozi katika maeneo inakotekelezwa miradi hiyo wanapaswa kuwa na uelewa wa kila hatua ya mradi ili watoe ushirikiano katika kuifanikisha.
“Jamii ikishirikishwa, itaichukulia miradi hiyo kwa umuhimu wa pekee na kutoa ushirikiano wa kila aina ili ifanikiwe. Tatizo lililopo ni kwa baadhi yenu kutowashirikisha wananchi hali inayosababisha wao kutokutambua faida ya miradi hiyo kwao, hivyo kutokutoa ushirikiano.”
Akieleza zaidi kuhusu aina ya ushirikishwaji unaopaswa kutolewa kwa wananchi, Wakili Kalolo alisema ni pamoja na kuwapatia viongozi wa vitongoji, vijiji, wilaya na mikoa, Mpango Kazi wa kila wiki, unaobainisha kazi ipi itafanyika kwa wakati upi ili waweze kufuatilia utekelezaji wake.
Alisema, kwa kuwashirikisha viongozi, wananchi wa maeneo husika wataweza pia kupata taarifa ya maendeleo ya miradi hiyo na wao kuwa sehemu ya ufuatiliaji wake.
Aidha, aliwataka Wakandarasi kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kuhusu kutumia vibarua wa maeneo inakotekelezwa miradi badala ya kuwatoa nje ya maeneo hayo.
Vilevile, aliwataka kujenga uhusiano mzuri na jamii kwa kulipia kwa wakati huduma zote zinazotolewa na wananchi ikiwemo vibarua, chakula na gharama za pango kwa nyumba wanazokodisha.
Katika hatua nyingine, Wakili Kalolo alilishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ushirikiano wake katika kusimamia utekelezaji wa miradi husika.
Alisema TANESCO ndiyo moyo wa REA kwani kwa uhalisia, miradi yote ya umeme inayotekelezwa kupitia REA, inapokamilika hukabidhiwa kwa TANESCO ili waendelee kuisimamia kwakuwa wao ndiyo wenye dhamana ya umiliki wa miundombinu ya umeme nchini.
Aliwataka Watendaji wa TANESCO hususan Idara ya Uhusiano kwa Umma kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa jamii kuhusu miradi ya umeme vijijini ikiwemo kufanya maandalizi ya kuunganishiwa umeme katika nyumba zao pamoja na matumizi ya vifaa vya Umeme Tayari (UMETA).
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti aliambatana na Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Amos Maganga pamoja na Wataalam mbalimbali kutoka TANESCO na REA.