Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mwanza
Mwanadamu hupewa jina ili kumtambulisha ili atofautishwe na watu wengine. Jina hilo
linaweza kuwa linamtambulisha yeye binafsi au cheo chake katika taasisi hata nafasi
yake katika nchi.
Siku ya Jumatano Agosti 08, 2021 itakumbukwa na Watanzania pamoja na dunia kwa
ujumla kwa kuwa Machifu wa Tanzania wamempata Chifu wao Mkuu wa kwanza
mwanamke ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan akichukua nafasi ya mtanglulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Kwa kukabidhiwa kwake madaraka hayo, kunamfanya apewe jina ambalo ndilo
linalomdhihirisha kuwa yeye ni Kiongozi Mkuu wa Kitaifa kuwaongoza Machifu wenzake
na Watanzania kwa ujumla.
Ilikuwa majira ya saa sita kuelekea saa saba mchana katika Viwanja vya Red Cross
eneo la Kisesa wilaya ya Magu mkoa wa Mwanza ndipo Mhe. Rais Samia alipewa jina
la Hangaya wakati alipokuwa anakabidhiwa madaraka ya kuwa Chifu Mkuu nchini.
Jina hilo, Hangaya lina maana ya nyota angavu ya asubuhi inayoonesha matumaini
linasadifu nafasi ya Mhe. Rais Samia ambayo Watanzania wana matumaini makubwa
kwa uongozi wake kwenye maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Ili kuwa Chifu kamili, Kiongozi huyo wa Machifu nchini, Chifu Hangaya alifanyiwa ibada
ya kimila iliyokuwa na sala maalumu ya kumuombea siha njema, dhima na dhamana ya
kuwa kiongozi hodari na mahiri kwa taifa analoliongoza.
Sala hiyo iliongozwa na maneno kuntu ambayo yalishamirisha sherehe hiyo adhimu
iliyokuwa imefurika hadhira iliyohudhuria Tamasha la Utamaduni la siku mbili kuanzia
Septemba 7 hadi 8, 2021. Tamasha hilo liliandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania
(UMT) kwa lengo la kulinda mila na desturi za Mtanzania liliongozwa na kaulimbiu
isemayo, “Turithishe Utamaduni Wetu, Tudumishe Utamaduni Wetu, Amani na Umoja ni
Tunu Zetu.”
Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Machifu Tanzania, Chifu Msagata wa Uchifu wa
Unyanyembe Tabora alisema “Sasa una mamlaka ya kuwaita watu kwa vikao vyako
kwa sababu una mamlaka, wewe ni kiongozi shupavu, imara, mkakamavu, mweledi,
uwaongoze watu wako kwa amani.”
Kiongozi huyo mpya amekabidhiwa vitendea kazi mbele ya jopo la Machifu na
Watanzania ikiwa ni alama ya kusimamia himaya yake ya kiutawala yaani Taifa la
Tanzania akisaidiwa na Machifu hao katika maeneo yao. Miongoni mwa vitendea kazi
hivyo ni pamoja na nguo nyeusi,nguo nyekundu, ngozi ya chui, ushanga ulio na yai la
mbuni, kiti cha utawala, ngao na mkuki pamoja na usinga.
Ili kujua maana ya vifaa hivyo, mwandishi wa makala haya alichukua wasaa wa
kuonana na Chifu Aron Mikomangwa Nyamilonda wa Uchifu wa Jiji la Mwanza
unaojumuisha Halmashuri za Ilemela na Nyamagana ambaye ni mbobezi wa masuala
ya utamaduni wa kabila la Wasukuma na kueleza kuwa, nguo nyeusi aliyovikwa Chifu
Hangaya ni alama ya mawingu meusi yanayoleta mvua ili wananchi walime na kupata
chakula. Chifu anapovaa nguo hiyo, maana yake Watanzania wanapomuona kiongozi
wao wanapata matumaini ya kupata mafanikio kupitia kiongozi wao chini ya uongozi
wake mahiri.
Aliendelea kusema kuwa, nguo nyekundu aliyovikwa Chifu Hangaya ni alama ya ulinzi,
Chifu Hangaya anapaswa kuilinda nchi yake. Kwa nafasi yake Rais ni mlinzi wa kwanza
wa nchi yake na watu wake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Kifaa kingine alichokabidhiwa Chifu Hangaya Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ni ngozi ya chui ambayo alivikwa ikiwa ni ishara na alama ya
upole na ulinzi wakati wote. Chifu Mikomangwa alisema “Muogope sana chui akiwa na
watoto wake ukimkanyaga atakumaliza.”
Kwa muktadha wa Rais Mhe. Samia kukabidhiwa madaraka hayo, yeye ndiye Chifu
Mkuu na chini yake wapo Machifu na Watanzania kwa ujumla wao ambao
wanamuombea awe mpole awe na mwangalifu kwa watu wote wenye nia ovu na
Tanzania.
Vile vile katika hafla hiyo Chifu Hangaya Samia alivikwa ushanga wenye yai la mbuni,
ndege huyo ni mwangalifu sana katika kulinda mayai na watoto wake. Hivyo,
Watanzania ndiyo mayai na vifaranga wa Chifu Hangaya Samia ambaye anawajibu wa
kuwalea, kuwatunza na kuwalinda Watanzania.
Hali kadhalika Mhe. Rais amekabidhiwa kiti chenye mguu mmoja ambacho ni alama ya
utawala mmoja ambacho hakikaliwi na mtu mwingine zaidi yake. Mikomangwa alisema
Hangaya anapokaa katika kiti chake cha kiutawala, hukaa na Watanzania ili kujenga na
kuendeleza nchi na watu wake.
Pia, amekabidhiwa ngao na mkuki akiwa kiongozi na Mkuu wa Mchifu nchini ili aweze
kulinda nchi yake na watu wake kupitia majeshi ya Ulinzi na Usalama ambapo yeye ni
Amiri Jeshi Mkuu.
Mwisho ila siyo kwa umuhimu, alikabidhiwa usinga unaotokana na singa za mikia ya
nyumbu ambao tafsiri yake ni watu. Usinga kwa muonekano na uhalisia wake una
manyoya mengi, haya yanawakilisha uwingi wa watu alionao Chifu Hangaya ambao ni
Watanzania. Amekabidhiwa ili awalinde kwa amani.
Hakika Chifu Hangaya Samia Suluhu Hassan ameanza kazi yake ya Uchifu mara moja
ambapo alisema Tanzania ipo kwenye mchakato wa kuandaa Sera mpya ya Utamaduni
itakayoendana na mazingira ya sasa ya dunia lakini itakayolinda maadili Mtanzania.
Hivyo, mara baada ya kukabidhiwa madaraka hayo aliagiza Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ndiyo yenye dhamana na Utamaduni kupata
maoni kutoka kwa Watemi na Machifu.
“Na niagize Wizara, katika maadalizi ya mchakato wa Sera hii, lazima tupate maoni
kutoka kwa Watemi na Machifu wetu, maoni yao yaingizwe kweye Sera hii ili tuendeleze
utamanuni wetu. Na ni imani yangu kuwa hatua hizi zitasaidia kulinda, kuenzi na kukuza
utamaduni wetu” alisisitiza Rais Mhe. Samia.
Ujio wa Machifu wengi katika hafla hiyo ya kukabidhiwa madaraka hayo kwa Chifu wao
Mkuu Hangaya Samia Suluhu Hassan ni udhihirisho na imani ya Watanzania wote
kusimama imara na kuhakikisha kaulimbiu ya uongozi wake ya “Kazi Iendelee” inakuwa
mwanzo mpya wa kuhakikisha utamaduni wa Mtanzania utaendelea kujulikana kote
kupitia filamu ya “Royal Tour” inayoandaliwa kuitangaza Tanzania duniani.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Filamu ya “Royal Tour”, Dkt. Hassan Abbasi
alisema kuwa filamu hiyo ni fursa adhimu ambayo itasaidia kutangaza rasilimali za
Tanzania huku akinukuu maneno ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alisema
“Baada ya kukamilika kwa filamu hii itakayotangaza utalii, biashara na fursa za
uwekezaji nchini kupitia kipindi maarufu cha Royal Tour, dunia itafahamu kuwa madini
ya Tanzanite yanachimbwa Tanzania pekee.”
Maneno hayo yalisemwa na Rais Septemba 5, 2021 akiwa mkoani Manyara wakati
akizungumza na wananchi wa Mirerani na kuongeza kuwa ni faraja na ushahidi dhahiri
kuwa eneo hilo ni mahali pekee yanakochimbwa madini ya Tanzanite duniani.
Sasa ni wakati wa kuutangaza utamaduni wa Mtanzania duniani ili kuakisi maneno ya
Mwasisi wa Taifa la Tanzania, Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere ambaye
aliwahi kusema “Utamaduni ni kiini ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na utamaduni ni
sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho.”
Kupitia Tamasha la Utamaduni la Kisesa Mwanza, Rais Mhe. Samia ametoa mwanga
na hamasa kwa makabila yote nchini kuanzisha matamasha katika maeneo yao ili
kutambulisha mila na desturi zilizopo katika maeneo yao na kutangaza fursa za
kiutamaduni na utalii hatua itakayosaidia kukuza uchumi katika mikoa yote na kila
pembe ya Tanzania.
Matamasha hayo yamekwisha anza kufanyika katika mikoa ya Mwanza, Arusha,
Manyara, Dodoma na Mbeya. Sasa ni zamu yenu mikoa mingine kuwa na matamasha
yanayowapa fursa ya kutangaza utamaduni wenu na kuwapa fursa Watanzania kufanya
utalii wa ndani katika mikoa yenu ili kuweza kujifunza mila, desturi, historia na tamaduni
za makabila mbalimbali yaliyopo nchini. “Hakika Kazi Iendelee.