Picha ya Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Arusha, Justine Masejo
****************************
Happy Lazaro, Arusha
Arusha.Watu watano akiwemo dereva wa gari wamepoteza Maisha katika ajali mbaya iliyotokea katika eneo la Konoike, Kikatiti, barabara ya Arusha Moshi Mkoani Arusha baada ya magari mawili kugongana uso Kwa uso .
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi Mkoani hapa kwenda kwa waandishi wa habari,iliyotolewa na Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Arusha,Justine Masejo alisema kuwa, tukio limetokea leo majira ya saa 10 Alfajiri ambapo gari aina ya Mitsubishi Fusso lenye namba T 111 CUU liligongana na gari jingine aina ya Mitsubishi Canter lenye namba T 612 BNN.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba gari aina ya Fuso lilikuwa likiendeshwa na dereva anayefahamika kwa jina la Heriel Lyimo (42) Mkazi wa Holili Mkoani Kilimanjaro huku gari aina ya Canter lilikuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Peter Mmasi ambaye umri na makazi yake bado hayajafahamika mara moja.
Uchunguzi wa awali inaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari aina ya Mitsubishi Fuso iliyokuwa inatokea Moshi kuelekea Arusha ambapo ilihama upande wa pili wa Barabara na kugongana na gari aina ya Mitsubish Canter lililokuwa linatokea Arusha kuelekea Mkoani Kilimanjaro.
Aidha baada ya magari hayo kugongana gari aina Mitsubish Fuso lilipitiliza na kuanguka
kwenye mtaro uliopo pembezoni mwa barabara.
Waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na dereva wa Gari aina ya Canter ,Peter Mmasi
Wengine ni Victor Kileo,Vivian Urio na Isack Temba ambao walikuwa abiria wa gari aina Mitsubish Canter na ni wakazi wa Baraa jijini Arusha.
Aidha katika gari aina ya Mitsubishi Fuso aliyefariki ni utingo wa gari hiyo aliyefahamika kwa jina moja la IDD mkazi wa Himo mkoani Kilimanjaro.
Majeruhi katika ajali hiyo ni Heriel Lyimo ambaye amepelekwa katika hospitali
ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi na miili ya marehemu imehifadhiwa katika
hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Jijini Arusha.