Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zinazoendelea kusambazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa makundi makubwa ya nyumbu wanaotumia maeneo ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, Eneo la Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro pamoja na maeneo ya Mapori ya Akiba ya Maswa, Ikorongo, Grumeti na Pori Tengefu la Loliondo yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Taarifa hizo sio za kweli tunaomba zipuuzwe. Ifahamike kuwa idadi ya nyumbu katika ikolojia ya Serengeti ilipungua kwa kiasi kikubwa kuanzia miaka ya 1890 hadi 1960 kutokana na vifo vilivyosababishwa na ugonjwa wa sotoka (rinderpest). Mwaka 1960 kulikuwa na nyumbu wapatao Laki moja na tisini elfu (190,000) kwenye mfumo Ikolojia Serengeti.
Aidha, idadi yao iliongezeka kwa kasi baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa kwa kuchanja mifugo ambayo ndiyo ilikuwa chanzo cha maambukizi kwa nyumbu, na ilipofika mwaka 1977 kulikuwa na nyumbu takribani milioni moja na laki nne (1,400,000). Aidha, ukame mkubwa uliotokea mwaka 1993 ulisababisha vifo vya wanyama wengi na kupunguza idadi ya nyumbu hadi kufikia laki tisa na kumi na saba elfu (917,000).
Hata hivyo, kufuatia hali nzuri ya malisho kwa miaka iliyofuata, idadi ya nyumbu iliongezeka hadi kufikia milioni moja na laki tatu (1,300,000) ilipofika mwaka 1998 na kuendelea kubakia kwenye wastani huo hadi mwaka 2015. Uongezekaji huu umechangiwa na kutokomezwa kwa ugonjwa wa sotoka duniani ilipofika mwaka 2011, na hivyo ugonjwa wa sotoka kuwa wa kwanza kutokomezwa katika magonjwa ya wanyama.
Kwa wastani, Sensa ya mwaka 1977 hadi 2015 inaonesha kuwa idadi ya nyumbu imefikia ukomo wa ongezeko kutokana na kiasi cha chakula kinachopatikana wakati wa msimu wa kiangazi kwenye mfumo wa Ikolojia Serengeti. Tafiti za nyumbu nchini zilizofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) zinaonesha kuwa idadi ya nyumbu imeendelea kubakia kileleni, takribani kati ya nyumbu milioni moja na laki mbili hadi milioni moja na laki tano kwa kadirio la juu.
Hivyo taarifa zinazoendelea kujadiliwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya jamii kuwa idadi ya nyumbu imepungua kwa asilimia 73% sio za kweli zina lengo la kuupotosha umma kuhusu idadi halisi ya nyumbu walio katika mfumo ikolojia wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Aidha, idadi ya nyumbu wanaovuka mpaka wa kimataifa na kuingia nchi ya jirani wakati wa kiangazi katika mzunguko wa kila mwaka (annual migration), inaonesha kutokuathiri idadi ya nyumbu wanaobakia Tanzania kwa muda mrefu ikilinganishwa na wanaovuka kwa kuwa idadi hiyo imekuwa ikipungua kutoka asilimia 50% miaka ya 1970 hadi kufikia 10-15% miaka ya hivi karibuni.
Utafiti umeonesha kuwa nyumbu wengi hubakia upande wa Tanzania kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kuimarika kwa ulinzi na uhifadhi wa makazi yao, upatikanaji wa malisho ya kutosha na maji katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Aidha, nyumbu wengi kwa sasa hawavuki kwenda upande wa pili wa mpaka wa Kimataifa na kuingia nchi jirani kutokana na ongezeko la shughuli za kibinadamu za kilimo, makazi ya watu, ukuaji wa miji, miundombinu, ujenzi wa uzio pamoja na changamoto ya mifugo kwenye nyanda za wanyamapori katika nchi jirani.