Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa ameshikilia mkuki na ngao ikiwa ni ishara ya kupewa madaraka ya kuwa Mkuu wa Machifu nchini wakati mara baada ya kufunga Tamasha la Utamaduni leo Septemba 08, 2021 Kisesa wilaya ya Magu mkoani Mwanza ambalo limeandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) lenye lengo la kulinda mila na desturi za mtanzania lililoongozwa na kaulimbiu ya “Turithishe Utamaduni Wetu, Tudumishe Utamaduni Wetu, Amani na Umoja ni Tunu Zetu.”
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa leo Septemba 08, 2021 Kisesa wilaya ya Magu mkoani Mwanza wakati wa Tamasha la Utamaduni ambalo limeandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) lenye lengo la kulinda mila na desturi za mtanzania lililoongozwa na kaulimbiu ya “Turithishe Utamaduni Wetu, Tudumishe Utamaduni Wetu, Amani na Umoja ni Tunu Zetu.”
**********************
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mwanza
Serikali imejipanga vema kuhakikisha inafungua na kuongeza wigo wa fursa za kuitangaza nchi kimataifa kwa kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii wa kiutamaduni vilivyopo hapa nchini.
Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati akifunga Tamasha la Utamaduni ambalo limeandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) lenye lengo la kulinda mila na desturi za mtanzania lililoongozwa na kaulimbiu ya “Turithishe Utamaduni Wetu, Tudumishe Utamaduni Wetu, Amani na Umoja ni Tunu Zetu.”
Akizungumza na wananchi na Watanzania, Mhe. Rais Samia amesema Utamaduni unasaidia kuendeleza mila na desturi njema za taifa letu, hatua ambayo ni msingi imara wa kuendeleza maadili ya Mtanzania kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine pamoja na kuendeleza amani nchini.
Utamaduni unahusisha mambo muhimu ambayo yanatamblisha Taifa letu duniani, akimnukuu Baba wa Taifa Mwl. Nyerere, Mhe. Rais amesema
“Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema, utamaduni ni kiini ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho,” amesema Rais Samia.
Kufuatia hatua hiyo, Rais Mhe. Samia ameyahamasisha makabila yote nchini kuanzisha matamasha katika maeneo yao ili kutambulisha mila na desturi zilizopo katika maeneo yao na kutangaza fursa za kiutamaduni na utalii hatua itakayosaidia kukuza uchumi katika mikoa yote na kila pembe ya Tanzania.
Akijibu hoja zilizotolewa na Uongozi wa Umoja wa Machifu nchini zikiwemo Machifu kutambuliwa rasmi, kupewa usajili wa kudumu pamoja na kupewa eneo makao makuu ya nchi Dodoma, Mhe. Rais amesema maombi yao yamepokelewa huku akiongeza kuwa hadi sasa Serikali imeanzisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo kwa mwaka huu wa fedha umepangiwa bajeti ya Sh. Bilioni 1.5 ili kusaidia maendeleo ya sekta hizo hapa nchini.
Akimkaribisha Mhe. Rais katika tamasha hilo, Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amemshukuru Rais kwa kuweka sekta ya Utamaduni kuwa miongoni mwa eneo ambalo linatambulisha utamaduni wa Mtanzania kimataifa kupitia programu ya kutangaza fursa za kuiuchumi zilizopo katika utalii wa kiutamaduni ziliopo hapa nchini.
Waziri Bashungwa ameongeza kuwa lengo la matamasha ya kiutamaduni yanayofanyika nchini ni kupata na kuendeleza maudhui ambayo yanatangaza nchi yetu duniani pamoja na fursa zilizopo kwenye utalii wa kiutamaduni ili kukuza na kuendeleza sekta hiyo nchini.
Tamasha hilo la Utamaduni limefana na kushamirishwa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbaliwa Serikali, viongozi wa dini, machifu kutoka maeneno mbalimbali nchini pamoja na wananchi kutoka mkoa wa Mwanza na mikoa jirani ikiwa ni hatua kuendeleza mila na desturi za Mtanzania pamoja na kuimarisha umoja na amani miongoni mwa jamii nchini.